Habari

Mimi si mtu wa ‘wantam’, atangaza mbunge Amina Mnyazi akisema atachaguliwa tena

Na PIUS MAUNDU July 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Malindi, Bi Amina Mnyazi, amewapa changamoto wanasiasa wanaopanga kushindania nafasi hiyo katika uchaguzi ujao, akisema maendeleo aliyofanikisha yanamweka pazuri kupata awamu ya pili ya uongozi.

Akiongea katika Shule ya Msingi ya Girimacha, Bi Mnyazi alikiri kuwa, ushirikiano kati ya Rais William Ruto na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, umesaidia kutekeleza miradi zaidi ya maendeleo.

“Hapo awali kiongozi alikuwa anapata mradi wa maendeleo kwa kujuana. Wanaotaka kushindana na mimi wana kazi sana kwa sababu nimewekeza katika miradi ya maendeleo,” alisema mbunge huyo aliye mwanachama wa ODM.

Wakati huo huo, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse amewataka magavana, wabunge na wawakilishi wa kike, waachilie fedha zote za basari ili kuongeza mgao unaoelekezwa kama ufadhili katika sekta ya elimu.

Bw Mutuse ameunga mkono Waziri wa Fedha John Mbadi ambaye alisema serikali haiwezi kuendelea kufadhili elimu kwa kulipa Sh22, 244 kwa kila mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.

Wiki jana, Bw Mbadi alisema kuwa bajeti ni kidogo na serikali inaweza tu kulipa Sh16,900.

Bw Mutuse amesema upungufu huo haujaanza na serikali hii na hata ulikwepo wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta wakati ambapo Dkt Fred Matiangí alikuwa waziri wa elimu.

Kufidia upungufu huo, Bw Mutuse amependekeza basari zote zijumuishwe kisha zielekezwe kufadhili elimu ya shule za sekondari.