Mirengo mitatu sasa yachipuka kupigania ubabe Mlima Kenya
ENEO la Mlima Kenya kwa sasa linakabiliwa na mtanziko ambao huenda ukasababisha mpasuko mkubwa kabla ya 2027 na kuliacha pasipo nguvu za kutosha kumng’oa Rais William Ruto kwenye debe.
Eneo hili linapania kuzamisha matumaini ya rais wa sasa kuongoza kwa muhula wa pili.
Kwa lengo la kujumuisha wapigaji kura takriban milioni nane kwa Uchaguzi Mkuu 2027, tanzu nne zenye nguvu zimechipuka ambazo huenda zikagawanya nguvu ya upigaji kura kiasi cha kudhoofisha eneo hilo kisiasa.
Kambi moja inaongozwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, ambaye amejitokeza kama kiongozi wa kisiasa kwa wanajamii Mlima Kenya.
Baada ya kutimuliwa Oktoba mwaka jana, Bw Gachagua alikataa kunyamazishwa kisiasa na kujikweza kuwa kinara wa upinzani anayehangaisha utawala wa Rais Ruto.
Bw Gachagua ametangaza anaungana na vinara wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, na Seneta wa Kisii Richard Onyonka.
“Rais na watu wake wamekuwa wakila njama za kututenga (Mlima Kenya). Hali hii imenichochea kwenda kusaka marafiki wa kushirikiana nao na habari njema ni kuwa, sasa tuna nafasi ya kumfanya mgombea wa pili kupoteza kwa nusu ya kura tutakazoshinda nazo,” alisema Bw Gachagua Jumapili iliyopita mjini Maragua, Kaunti ya Murang’a.
Kambi nyingine inaongozwa na Rais Ruto binafsi anayeshirikiana na Naibu Rais Kithure Kindiki.
Kambi ya tatu inayochipuka inaongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye bado anatambulika kama kigogo wa eneo hilo.
Chama cha Bw Kenyatta, Jubilee awali kiliegemea Bw Musyoka lakini baadaye kikamuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama wa ndani, Dkt Fred Matiang’i, ambaye ameelezea azma ya kuwania urais.