Mkakati wa upinzani ukiungana dhidi ya UDA uchaguzi mdogo Malava
UPINZANI umeonyesha umoja wa kweli baada ya mgombeaji wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Malava kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho ili kumuunga mkono Seth Panyako, mgombea wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).
Edgar Busiega alitangaza kujiondoa kwake baada ya mashauriano ya kina kati ya viongozi wa vyama washirika vya upinzani, hatua inayolenga kudhoofisha nafasi ya mgombea wa chama tawala cha UDA, anayepigiwa debe na Rais William Ruto.
Hatua hiyo imechukuliwa kama pigo kwa kambi ya UDA inayoongozwa na Musalia Mudavadi, Farouk Kibet na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ambao wameweka nguvu zao zote katika kampeni hizo.
Naibu kiongozi wa chama cha DCP Cleophas Malala alisema uamuzi huo ni ushindi mkubwa kwa upinzani na kwa Panyako binafsi.
“Uamuzi wa ndugu yangu Busiega kujiondoa kwa hiari ni wa kishujaa. Malava ni kubwa kuliko mtu mmoja. Tukija pamoja, tunaweza kushinda mradi wa utawala kandamizi,” alisema Malala.
Busiega alisema kujiondoa kwake ni uamuzi mgumu zaidi maishani mwake, lakini alifanya hivyo kwa ajili ya umoja wa jamii ya Waluhya.
“Nilitamani kuwa mbunge wa Malava, lakini nimegundua si wote tunaweza kuwa viongozi kwa wakati mmoja. Nitaunga mkono Panyako kwa moyo wote,” alisema.
Aliongeza kuwa alikutana na viongozi wa DAP-K na DCP, George Natembeya na Rigathi Gachagua, ambapo walikubaliana kuimarisha umoja wa upinzani.
“Uamuzi wangu ni mwanzo wa umoja wa kweli wa Waluhya. Leo tumeonyesha kwamba umoja huu unawezekana,” alisema Busiega.
Kwa upande wake, Malala alisema DCP imemuahidi Busiega nafasi ya kwanza ya uteuzi wa ubunge mwaka 2027 kama shukrani kwa kujitolea kwake.
“Baada ya kufanya utafiti wa kitaalamu, tuligundua kuwa Panyako ndiye mgombea mwenye nguvu zaidi, na kwa hivyo tuliamua kumuunga mkono,” aliongeza.
Panyako, ambaye pia ni afisa wa Chama cha Wauguzi (KNUN), alisema muungano huo ni mwanzo wa safari ya kuunganisha watu wa magharibi mwa Kenya.
“Ushindi wa upinzani utakuwa ushindi wa watu wa Malava na fahari ya jamii ya Waluhya,” alisema.
Alishukuru Busiega na chama cha DCP kwa kujitoa na kumuunga mkono, akifichua kuwa alikataa ofa kutoka UDA na ODM kwa sababu alitaka “heshima ya jamii yetu ihifadhiwe.”
Kujiondoa kwa Busiega kunawaacha wagombea wanane katika kinyang’anyiro hicho, akiwemo Seth Panyako (DAP-K), David Ndakwa (UDA), Wilberforce Tuvei (Kenya Moja), James Angatia (ARC), George Oyugi (PDU), Bruce Shivakale (EPP), Benjamin Nalwa (NUPEA) na Joab Manyasi (DNA).
