Habari

Mkanganyiko uliopelekea Kadinali Njue kutoshiriki zoezi la kuchagua Papa mpya

Na ELVIS ONDIEKI May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KADINALI John Njue hatahudhuria baraza maalum la makadinali kumteua Papa mpya kutokana na sababu za kiafya na wala sio kwa kukosa mwaliko, Kanisa Katoliki limefafanua.

Askofu Mkuu Nairobi, Philip Anyolo, amesema licha ya Kadinali Njue kuhitimu kupiga kura (kwa kuwa na umri wa chini ya miaka 80 Papa Francis alipokufa) hatakuwa miongoni mwa makadinali zaidi ya 130 watakaopiga kura kesho kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki.

“Kwa kujibu maswali kadhaa kuhusu iwapo Kadinali John Njue atashiriki kikao cha baraza kitakachoanza Mei 7, 2025, nathibitisha sasa kwamba japo amehitimu kushiriki na alialikwa rasmi kupitia Mwakilishi wa Papa Kenya, kuambatana na Afisi ya Askofu Mkuu Nairobi, na kwa kuwasiliana na Makao Makuu ya Kanisa la Kikatoliki kwamba, kutokana na hali yake sasa kiafya, Kadinali John  Njue hataweza kusafiri Roma na kushiriki baraza maalum la makadinali wa kumteua papa,” alisema Askofu Anyolo kupitia taarifa.

Kadinali Njue aliambia Taifa Leo Jumatatu kuwa hakualikwa.

Kituo rasmi cha mawasiliano ya Kanisa Aprili 29, kilisema japo kuna makadinali 135 waliohitimu kupiga kura, “wawili wamethibitisha hawataweza kuhudhuria Baraza maalum kwa sababu za kiafya na kupunguza idadi kuwa 133.”

Baada ya udadisi, shirika la habari la Kikatoliki, Catholic News Agency, lilifichua wawili hao ni Kadinali Njue na Kadinali Antonio Cañizares wa Uhispania.

Taarifa ya Anyolo ilisema, “makadinali wanapojiandaa kuingia baraza Jumatano, ninawahimiza kwa dhati waumini wote kuomba kwamba Roho Mtakatifu atawaelekeza makadinali wanaposhiriki wajibu muhimu wa kumteua Baba Mtakatifu, atakayechunga Kanisa la Ulimwengu, tuzidi pia kuombea afya njema ya Kadinali John Njue.”

Kushiriki kwa Kadinali Njue kumekuwa suala tata. Kwenye tovuti ya Makao Makuu ya Kanisa la Kikatoliki, katika wasifu ulioandikwa upya mara ya mwisho 2014, tarehe yake ya kuzaliwa inaashiria 1944.

Hata hivyo, ripoti mpya zilizotolewa na Catholic News Agency zilisema umri wake “ulirekebishwa majuzi” na Vatican kuwa Januari 1, 1946.

Hatua hiyo inamfanya kuhitimu kumpigia kura papa mpya hadi Januari 1, 2026.