Mkasa wa maporomoko ya ardhi waikumba Pokot Magharibi
Na OSCAR KAKAI
MIILI 12 ikiwemo ya watoto saba imepatikana huku kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi Apollo Okello akisema walioangamia kwenye maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua iliyopitiliza Ijumaa usiku ni watu 24.
Bw Okello amesema shughuli za kiutu zingali zinaendelea maeneo yaliyoathirika.
Mvua ilisababisha uharibifu mkubwa ambapo sehemu ya barabara ya Kitale-Lodwar karibu na Ortum imekatika na kufanya kuwa vigumu kuvifikia kwa usafiri wa barabarani vijiji vilivyoathirika vya Nyarkulian na Parua.
Daraja la Muruny limeharibiwa na maji hayo ya mafuriko.
Mapema Jumamosi ilihofiwa angalau watu 16 walikuwa wameangamia baada ya mvua iliyopitiliza kusababisha maporomoko ya ardhi na kufagia nyumba zao Ijumaa usiku katika Kaunti ya Pokot Magharibi, kulingana na maafisa.
Hata hivyo, idadi hiyo imepanda.
Msimamizi mmoja wa masuala ya utawala, Joel Bulal, alikuwa ameambia Taifa Leo kwamba watu si chini ya 12 walizikwa wakiwa hai kijijini Nyarkulian na wengine wanne katika kijiji cha Parua.
Bw Bulal alisema shughuli za uokozi zinaendelea tangu asubuhi ili kuwapata ama wahanga au manusura wa mkasa huo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema tayari timu yake ya uokozi imechukua hatua na inawajibika.