Mkataba wa serikali ya mpito watiwa saini Sudan, azimio la kikatiba lapatikana
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta ameungana na viongozi wa mataifa mengine ya Afrika kushuhudia kutiwa saini mkataba wa serikali ya mpito ukijumuisha “azimio la kikatiba” linalotoa fursa kuhamia kwa utawala wa kiraia nchini Sudan.
Mkataba huo uliotiwa saini Jumamosi unakomesha mvutano mkali ambao umekuwa ukiendelea kati ya raia na wanajeshi nchini humo kwa miezi kadha tangu kuondolewa mamlakani kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Omar al-Bashir mnamo Aprili 2019.
Rais Kenyatta alipongeza Baraza la Kijeshi la Utawala wa Mpito (TMC) na upinzani kwa kukubali kugawana mamlaka, hatua ambayo itatoa nafasi ya uchaguzi wa kidemokrasia baada ya miezi 39, akisema viongozi wa mirengo hiyo wameweka mbele masilahi ya kitaifa badala ya masilahi yao.
“Ninawashukuru kwa kuweka masilahi ya raia mbele na kukubali kujadiliana kwa ajili ya kudumisha amani,” Rais Kenyatta amesema wakati wa hafla ya kutiwa saini kwa mkataba huo iliyofanyika katika mkahawa wa Corinthia jijini Khartoum.
Kiongozi wa taifa aliwahakikishia viongozi wa kijeshi wanaoongoza Sudan na raia wa nchini humo kwamba Kenya itasimama nao wanapoanza safari kuelekea utawala wa kidemokrasia.
Rais Kenyatta pia aliwataka raia wa Sudan kusuluhisha masuala kinzania yaliyosalia kwa njia ya mazungumzo huku wakiheshimu utawala wa kisheria.
“Amani na usalama ndio msingi ambako masuala hayo yote yatajengwa. Mataifa ya eneo hilo na jamii ya kimataifa yako tayari kuwasaidi kujenga taasisi thabiti za utawala,” akasema Rais Kenyatta akiongeza kuwa uwepo wa amani nchini Sudan ni wa manufaa kwa eneo hili na Afrika kwa ujumla.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais Salva Kiir (Sudan Kusini), Rais Idriss Deby Itno (Chad) na Rais Faustin Archange Tuadera (Jamhuri ya Afrika ya Kati).
Wengine walikuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Faki Mahamat.
Rais Kenyatta aliandamana na Waziri wa Masuala ya Kigeni Dkt Monica Juma.
Mkataba huo wa ugavi wa mamlaka ulitiwa saini na Naibu Mkuu wa Baraza la Kijeshi Linalotawala Mohamed Hamdan Daglo na mwakilishi wa Alliance for Freedom and Change – kinacholeta pamoja waandamanaji – Ahmed al-Rabie, kwa mujibu wa ripota wa AFP.
Chini ya mkataba huo, idadi kubwa ya raia watashirikishwa katika serikali ya mpito inayoongozwa na baraza hilo la TMC.
Na serikali hiyo mpya itatangazwa “siku chache baada ya kutiwa saini kwa mkataba huu wa amani”.
Waziri Mkuu anatarajiwa kutajwa Agosti 20 huku baraza jipya la mawaziri likizunduliwa wiki moja baadaye, yaani mnamo Agosti 28.