Habari

Mke amshtaki mume kwa ulaghai wa penzi

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 30, ameshtakiwa na mwanamke kwa kumuoa akijua kwamba alikuwa na mke mwingine.

Bi Neema Nijnikant Shah, anadai kwamba George Gona Charo alimuoa akijua kwamba alikuwa mume wa Bi Dama Kaingu.

Kulingana na mashtaka, Bw Charo analaumiwa kwa kumuoa Bi Neema kupitia harusi ya kijamii katika mkahawa wa Shenai mjini Mombasa akijua kwamba alikuwa na mke mwingine. Sheria ya ndoa ya Kenya hairuhusu mtu kuoa au kuolewa kabla ya kumtaliki mke wa kwanza.

Bw Charo pia anakabiliwa na shtaka la kutoa habari za uongo. Kulingana na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, mshtakiwa alimdaganya msajili wa ndoa kwamba hakuwa ameoa alipokuwa akiandaa harusi na Bi Neema.

Mashtaka yanasema kwamba mshukiwa alimweleza msajili wa ndoa kwamba hakuwa ameoa, habari ambazo alijua au aliamini zilikuwa za uongo. Shtaka linaeleza kwamba alinuia kumfanya msajili kufungisha ndoa jambo ambalo hangefanya iwapo angefahamu ukweli.

Katika shtaka la tatu inadaiwa kwamba alitisha kumuua mlalamishi alipogundua kwamba alikuwa na mke mwingine.

Inasemekana kwa muda aliokuwa akimchumbia Bi Neema hakumfichulia kwamba alikuwa ameoa.

Kwenye ushahidi wake, Bi Neema alisema alifanya harusi na mshtakiwa na baadaye akagundua alikuwa mke wa pili. Alieleza kuwa wakati mmoja walienda kubarizi Mauritius.

Alisimulia kuwa mnamo 2016, alienda nyumbani mashambani kwa mshtakiwa eneo la Kaloleni ambako walikuwa wamejenga nyumba.

“Charo alipotoka ndani ya nyumba hakunisalimia. Alikuwa mkali na kuniuliza kwa nini sikumfahamisha kuhusu ziara yangu. Sikumjibu, nilinyamaza tu,” alisema.

Mwanamke huyo alisema badala ya kujibu salamu zake, mshtakiwa alianza kumtusi na kutisha kumchoma kwa petroli.

Alisema aliamua kurudi katika nyumba yake mtaani Nyali anakoendesha biashara.

Alisema Charo alimuonyesha mwanamke mwingine mama ya watoto watatu aliyedai alikuwa mke wake. “Nilishangaa kwa sababu ni mimi niliyefadhili ujenzi wa nyumba hiyo. Nilijitahidi kuhakikisha tulijenga nyumba Kaloleni,” alisema.

Alisema kabla ya kuoana alikuwa amemwajiri Charo katika kampuni yake kama meneja lakini baada ya kumpata alikuwa na mke mwingine uhusiano wao uliharibika.

Alisema baada ya kutisha kumuua, Charo aliacha kufika nyumbani kwao Nyali baada vitisho alivyotoa Kaloleni.

Alisema alitafuta msaada wa pasta wao kuwapatanisha lakini haikuwezekana.

“Mshtakiwa alifika nyumbani baada ya pasta kuzungumza naye lakini hakunikaribia kitandani wala kunisemeza,” alisema.

Alisema Charo aliondoka kwenda Nairobi bila kumfahamisha na akaripoti kwa polisi ili achukuliwe hatua. Kesi itaendelea Juni 11.