Mkenya Phoebe Okowa achaguliwa jaji wa Mahakama ya Kimataifa
MWANASHERIA na msomi wa Kenya Profesa Phoebe Okowa amechaguliwa kuhudumu kwa muhula kamili wa miaka tisa kama jaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki (ICJ), baada ya kushinda uchaguzi mkali uliohusisha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) na Baraza la Usalama.
Profesa Okowa mwenye umri wa miaka 61 alipata ushindi huo katika duru ya tatu ya kupiga kura iliyofanyika katika makao makuu ya UN jijini New York Jumanne.
Katika kura ya mwisho, alipata kura 183 kati ya nchi wanachama zilizoshiriki, huku mpinzani wake wa mwisho kutoka Peru, Luz del Carmen Ibáñez Carranza, akipata kura mbili pekee. Nchi sita hazikupiga kura.
Pia aliungwa mkono kwa wingi katika Baraza la Usalama la UN, baada ya kukosa kufikia kiwango hicho katika duru ya awali alipopata kura sita pekee kati ya 15.
Okowa tayari alikuwa akihudumu katika mahakama hiyo tangu mwaka jana, alipochaguliwa kukamilisha muhula wa jaji kutoka Somalia Abdulqawi Ahmed Yusuf, aliyejiuzulu kabla ya muda wake kumalizika Januari 2027.
Ushindani wa wadhifa huo uligeuka kuwa wa Afrika baada ya Muungano wa Afrika kushindwa kuwashawishi Okowa na mwanasheria wa Sierra Leone Charles Chernor Jalloh kujiondoa.
Katika duru ya pili, Okowa alipata kura 89 katika Baraza Kuu, lakini hakuchaguliwa kwa sababu hakuwa amepata uungwaji mkono unaohitajika katika Baraza la Usalama. Jalloh alipata kura 30.
Baadaye Jalloh na wagombeaji wengine wawili, Paik Jin-Hyun wa Korea Kusini na Marcelo Vázquez-Bermúdez wa Ecuador, walijiondoa, na kuacha mgombeaji wa Peru na Okowa wakipambana katika duru ya mwisho.
Uchaguzi wa majaji wa ICJ unahitaji mgombeaji kupata kura nyingi katika Baraza Kuu na Baraza la Usalama kwa wakati mmoja.
Okowa ni mtaalamu wa sheria za kimataifa na amewahi pia kuhudumu katika Tume ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa.
Ingawa Kenya ilifanya kampeni kubwa kumuunga mkono, Okowa hatahudumu mahakamani kama mwakilishi wa nchi yake. Atakuwa huru kufanya maamuzi kulingana na sheria na wajibu wake wa mahakama, hata katika kesi zinazohusu Kenya.
Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei alisema utaalamu wa Okowa utasaidia mahakama hiyo kuendeleza mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria.
ICJ ina majaji 15 na jukumu lake kuu ni kusikiliza mizozo kati ya mataifa. Pia inaweza kutoa ushauri wa kisheria kwa ombi la Baraza Kuu la UN.
Mahakama hiyo ni tofauti na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo hushughulikia kesi za watu binafsi wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa wa kimataifa.