Siasa

Korti yampa Mbunge wa Mosop Abraham Kirwa siku 5 kueleza kwa nini kiti chake kisitangazwe kuwa wazi

Na BENSON MATHEKA November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Mosop Abraham Kirwa amepewa siku tano kueleza sababu za kutohudhuria vikao vya Bunge kwa zaidi ya miaka miwili, katika kesi inayolenga kiti chake kitangazwe kuwa wazi.

Jaji Roselyne Aburili wa Mahakama Kuu aliruhusu Kirwa na Spika wa Bunge la Kitaifa kujibu madai ya mpigakura Timothy Tororey kwamba wakazi wa Mosop wameachwa bila uwakilishi wa kutosha.

Jaji aliagiza mbunge huyo na Spika kuwasilisha majibu na hoja zao za maandishi ndani ya siku tano kuanzia Novemba 2, 2026.

Tororey naye amepewa siku tano baada ya kupokea majibu hayo kuwasilisha stakabadhi na hoja za ziada.

Tororey, mkazi na mpigakura wa Mosop, anadai Kirwa amekuwa nje ya nchi kwa muda mrefu na kukosa vikao na shughuli rasmi za Bunge.

Anasema hali hiyo imewanyima wakazi nafasi ya kuwakilishwa katika mijadala, kupiga kura na maamuzi kuhusu matumizi ya rasilimali za taifa.

Pia anamlaumu Spika kwa kushindwa kuchukua hatua, akisema sheria inaruhusu kiti cha mbunge kutangazwa wazi iwapo atakosa vikao vinane mfululizo bila ruhusa.

Hata hivyo, Spika kupitia Karani wa Bunge Samuel Njoroge alisema Kirwa alipata ruhusa ya kutohudhuria vikao kwa sababu za kiafya ili kupata matibabu nje ya nchi.

Kirwa pia alisema alikuwa akisafiri kutafuta matibabu na alikuwa amepata idhini ya Spika. Alidai hakuwahi kupewa rasmi stakabadhi za kesi hiyo, bali aliifahamu kupitia Bunge.

Akikubali ombi lao Jaji Aburili alisema suala hilo linaweza kuathiri hatima ya mbunge aliyechaguliwa na wananchi, hivyo ni muhimu asikilizwe kabla ya uamuzi wa mwisho.

“Maamuzi yanayoombwa yanaweza kuathiri muda wa kuhudumu kwa mbunge aliyechaguliwa na, kwa upana zaidi, wapigakura anaowawakilisha,” alisema.