Habari

Mkenya Phoebe Okowa achaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Na CHARLES WASONGA November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imechangamkia kuchaguliwa kwa Mkenya Profesa Phoebe Okowa kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Akitoa tangazo hilo Novemba 12, 2025, Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei  alisema ushindi huo unatokana na ujuzi mkubwa alionao Profesa Okowa na nafasi kuu ambayo Kenya inashikilia katika fani ya sheria ya kimataifa.

Dkt Sing’oei alieleza, kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, kwamba Profesa Okowa alitangazwa mshindi baada ya awamu ya nne ya upigaji kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

“Baada ya awamu nne ya upigaji kura, Profesa Phoebe Okowa amechaguliwa rasmi na UNGA na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kama jaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki, akiwashinda wagombeaji wengine watatu,” akasema.

Dkt Sing’oei pia alitambua mchango wa wanadiplomasia wa Kenya katika miji ya New York (Amerika) na Geneva (Uswizi) kwa kuongoza kampeni iliyofanikisha ushindi.

“Ushindi huo pia unaonyesha imani ya asasi hizo kwa uweledi wa kisheria wa Profesa Okowa na hadhi ya Kenya. Napongeza makundi yetu katika miji ya New York na Geneva kwa kuongoza kampeni kwa bidii,” akaeleza.

Profesa Okowa alipata kura 106 kati ya 185 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), na kuzidi kura 97 zinazohitajika kwa mgombeaji kutangazwa mshindi.

Vile vile, alizoa kura nane kati ya 15 katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), idadi inayohitaji kwa mgombeaji kupata ushindi.

Kiti hicho cha Jaji wa ICJ kilisalia wazi kufuatia kujiuzulu kwa Jaji Abdulqawi Ahmed Yusuf, raia wa Somalia mnamo Septemba 30, 2025.

Profesa Okowa ni wakili na Profesa katika kitengo cha Sheria ya Kimataifa.

Wakati huu anafundisha katika Chuo Kikuu cha Queen Mary University of London, nchini Uingereza.