Mkewe Rais akiri ahadi za viongozi hukinzana na uhalisia wa mambo nyanjani
MKE wa Rais William Ruto, Bi Rachel Ruto amekiri ahadi nyingi za wanasiasa wakati wa kampeni haziakisi uhalisia wa hali mashinani.
Akizungumza Kaunti ya Kilifi, Bi Ruto alikiri kwamba kusuluhisha kero la uhaba wa maji katika eneo kame la Ganze ni muhimu katika ustawishaji wa mpango wa bustani ya jikoni.
Bi Ruto alizuru Ganze kusherehekea maendeleo kwenye vita vya kuangamiza njaa na kupigia debe mradi wake kwa jina ‘Lisha Mmoja, Angamiza Njaa’.
Hata hivyo, alikumbana na kilio cha wakazi na wasimamizi wa shule waliosema mpango huo wenye nia njema huenda usifaulu kutokana na kero la ukosefu wa maji ambalo limehangaisha eneo hilo kwa muda mrefu.
Katika hafla ya kuwapa maziwa wanafunzi wa Shule za Msingi za Kachororoni na Gandini, Mama Taifa alikiri kwamba licha ya ahadi zenye nia njema kutoka kwa viongozi, uhalisia uliopo mashinani unaweza ukazuia utekelezaji.
“Wakati mwingine tunazunguka nchi tukitoa ahadi lakini uhalisia ni kuwa, chochote tunachosema hakiwezi kufanya kazi. Naweza kuahidi kuchimba visima chungunzima lakini vikauke au maji yawe ya chumvi,” alisema.
Aliahidi kukutana na viongozi wa Kilifi kujadili mikakati ya muda mrefu ya kusuluhisha kero la ukosefu wa maji pasipo kupunja raslimali za umma.
“Tutapata maji lakini namna ya kufanikisha jambo hilo, ndiyo tunataka kujadili na kaunti, serikali kuu na afisi yangu kupata suluhisho la kudumu – siyo la muda mfupi, kisha tusonge mbele,” alisema.
Jamii ya Ganze inayotegemea pakubwa vituo vya maji vinavyojazwa wakati wa msimu wa mvua ina mifereji michache ya maji.
Vua zinazobadilika badilika zimeathiri mazao na kusababisha wanajamii kutegemea msaada kutoka kwa serikali na wahisani.
Japo shule hizo mbili zimeanzisha bustani za jikoni, ukosefu wa maji umefanya kuwa vigumu kuzistawisha huku mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Gandini, Bi Hellen Mwaringa, akitoa wito kuwepo suluhisho la kudumu.
“Suluhisho la kudumu kuhusu maji ni muhimu kustawisha bustani za jikoni, kuimarisha usafi na kuhakikisha ufanisi wa mradi,” alisema.
Mbunge wa Ganze, Bw Kenneth Kazungu, aliangazia hali ya eneo hilo kutengwa kwa miaka mingi na kuorodheshwa miongoni mwa maeneobunge fukara.
“Watoto wa Ganze ni werevu sana lakini ufukara ndilo tatizo kuu. Wengi huenda shule bila kula chochote na kushindwa kumakinika kwa sababu wanawaza kila mara kuhusu matatizo yaliyopo nyumbani,” alisema.
Naibu Gavana wa Kilifi, Bi Flora Chibule aliwahimiza wanajamii kutumia maji yanayomwagwa ili kustawisha bustani wakisubiri suluhisho za kudumu.
Hatima ya bustani za jikoni zilizozinduliwa mapema mwaka huu katika shule za msingi za Kachororoni na Gandini sasa inategemea jinsi maeneo hayo yatakabiliana na kero la ukosefu wa maji.