HabariHabari za Kaunti

Msipowaanika baba wa kambo ‘mafisi’, mambo yataenda kombo – MUHURI

Na KALUME KAZUNGU August 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAHARAKATI wa kijamii Kaunti ya Lamu wamelalamikia tabia ya baadhi ya wakazi wanaoficha visa vya dhuluma za kingono nyumbani.

Wanaharakati hao, wakiongozwa na Mshirikishi wa Shirika la kutetea kaki za binadamu la Muslims for Human Rights (MUHURI) tawi la Lamu, Bw Mohamed Skanda, walifichua kuwepo kwa kesi ambapo baba wa kambo wamekuwa wakiwanyemelea wasichana wao wa kambo na kuwanajisi.

Bw Skanda pia alitaja hulka ambapo ndugu wa kambo wamekuwa wakishiriki ngono ya lazima na akina dada wao wa kambo ila visa hivyo haviripotiwi.

Akizungumza kwenye kongamano la kijamii kwenye ukumbi wa Lamu Fort, Bw Skanda alieleza haja ya jamii kuepuka tabia ya kuficha uhalifu kila unapotokea nyumbani.

Aliwataja kina mama kuwa mstari wa mbele kuficha uhalifu kama unajisi au uchafuzi unapotekelezwa kwa wasichana wao na akina baba kwa kuhofia waume wao kushikwa na kufungwa.

“Visa vya akina baba kuwabaka wasichana wao, hasa wale wa kambo zimekithiri hapa kisiwani na Lamu kwa jumla. Ila akina mama wamekuwa wakidinda kuripoti visa hivyo kwa kuhofia waume wao ambao ndio wanaoleta unga nyumbani kushikwa na kukabiliwa na mkono wa sheria. Wakati umewadia kwetu kama jamii kujitokeza kuwasema wahalifu hao,” akasema Bw Skanda.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Khadija Bakari aliyesisitiza haja ya jamii kujitenga na uhalifu kwa kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kushtakiwa.

Bi Bakari aidha aliwasihi wanandoa kujiepusha na kutengana akisema punde hali hiyo inapotokea watoto ndio huumia.

“Ukitazama matukio mengi ya wahalifu wanaotiwa mbaroni kwenye jela zetu, utapata ni za wale waliopokea malezi ya mzazi mmoja. Tujiepushe na talaka na kuhakikisha watoto wetu wanakua katika mazingira ya baba na mama. Tukifanya hivyo tutapunguza uhalifu katika jamii,” akasema Bi Bakari.

Wanaharaati hao pia walisisitizia idara ya usalama kukaza kamba kwa kuhakikisha kila anayejihusisha na visa vya uhalifu, hasa unajisi, uchafuzi na ulawiti anakamatwa na kuandamwa na mkono wa sheria.