Habari

Mkuu wa huduma za feri akatazwa kutumia eneo la VIP kivukoni Likoni

July 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

KULIKUWA na kizaazaa katika kivuko cha Likoni Ijumaa baada ya afisa mmoja wa polisi kumkataza mkurugenzi mkuu wa Shirika la Huduma za Feri Nchini (KFS) Bakari Gowa kutumia njia wanayotumia maafisa wa serikali na wale wa shirika hilo kivukoni hapo.

Afisa huyo wa kike mwenye cheo cha inspekta amesimamisha gari la Bw Gowa na kuamuru lirudishwe nyuma alipokuwa anaelekea kwenye feri.

Kisa hicho kimetokea upande wa Likoni ambapo Bw Gowa alikuwa na gari lake jeusi.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho afisa huyo ambaye amesemekana kujipiga kifua anapokuwa kazini, amemkataza Bw Gowa akisema “niko kazini”.

Amefanya hilo muda tu baada ya kuruhusu gari moja la polisi ambalo lilikuwa mbele ya lile la Bw Gowa.

Hali hiyo ilimkasirisha Bw Gowa na kumlazimu kushuka na kukabiliana na afisa huyo akiumueleza kuwa yeye ni msimamizi wa huduma hizo.

“Afisa huyo alisema hataki kuelewa kwani alikuwa kazini kwa hiyo alitaka Bw Gowa asonge kando kabla ya kuongea,” amesema mmoja wa wale walioshuhudia kisa hicho.

Bw Gowa anasemakana kushuka akiwa amejawa na hasira na kumshambulia afisa huyo akimueleza ambavyo baadhi ya maafisa wa polisi wamekuwa wakinyanyasa wafanyakazi wa KFS kutumia njia hiyo.

Watu wenye vibali kutoka kwa KFS huruhusiwa kutumia njia hiyo ambayo ukiwa upo na gari unaweza usipange laini kusubiri feri.

“Bw Gowa alikuwa mkali sana kwa sababu alikuwa amesikia jinsi ambavyo watu wanadhalilishwa hapa,” amesema afisa mmoja wa KFS aliyekuwa hapo.

Hali hiyo ilisababisha maafisa wengine kuja hapo kabla ya kumtambua Bw Gowa na baadaye kumuachilia kuelekea kule alikokuwa anaelekea.

Maafisa wa polisi wamekuwa kivukoni hapo kwa miezi mitatu sasa tangu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa watakuwa wanasaidia huduma hizo.

Kuja kwao kulisababisha fujo mara ya kwanza wakati waliwachapa watumia wa feri na baadaye hali ikawa shwari.

Kwa upande mwengine kuwepo kwa maafisa hao kumesaidia kuwepo kwa nidhamu kivukoni hapo ambapo kunajulikana kuwa na msongamano wa mara kwa mara.