Habari

Mlima kwa Uhuru 2020

January 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

MWAKA huu wa 2020 unaanza Wakenya wakimtazama Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kuwahakikishia kwamba utakuwa bora kwao kuliko walioaga Jumanne wa 2019.

Kiongozi wa nchi anakabiliwa na wakati mgumu kudumisha umoja na uthabiti nchini, serikalini, katika chama tawala cha Jubilee na kuzima joto la kisiasa huku uasi ukiongezeka, hasa katika ngome yake ya eneo la Mlima Kenya.

Kiuchumi, serikali iliwavunja moyo Wakenya na Rais Kenyatta atajikuna kichwa kuhakikisha kuwa 2020 utakuwa mwaka tofauti na ilivyokuwa 2019.

Ukiwa mwaka wa tatu wa kipindi cha pili cha utawala wake, Rais Kenyatta atalazimika kuhakikisha sera za serikali yake zitapunguzia Wakenya gharama ya maisha ambayo mwaka ulikamilika ikiwa asilimia 5.85

Hii itakuwa ni mlima kwake ikizingatiwa kwamba, Kenya ina madeni ya kima cha Sh6 trilioni inayopaswa kuanza kulipa mwaka 2020 na serikali inapanga kukopa Sh3 trilioni zaidi.

Mbali na kulipa madeni, serikali itahitaji pesa za kufadhili bajeti yake ambayo ina pengo la Sh637 bilioni.

Mwaka 2020, inapanga kukopa Sh331 bilioni kutoka wafadhili wa kigeni na Sh305.7 bilioni kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini.

Hii inamaanisha kuwa, serikali ya Rais Kenyatta itakuwa na wakati mgumu kulipa madeni bila kuongezea Wakenya, ambao wamelemewa na gharama ya maisha, ushuru zaidi.

Miradi kadhaa ya serikali ukiwemo utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu na Ajenda Nne Kuu inahitaji pesa na itakuwa vigumu serikali kuepuka kuongeza ushuru mwaka 2020.

Mwaka 2019 serikali ililazimika kupunguza bajeti za wizara na baadhi ya idara zake, ikiwemo ya mahakama ili kupata pesa za kufadhili miradi ya Ajenda Nne Kuu.

Ingawa Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa wakati wa siasa ulipita, mdahalo kuhusu utekelezaji wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), unatarajiwa kupandisha joto la siasa.

Tayari, uasi umezidi katika ngome yake ya Mlima Kenya, baadhi ya wabunge wanaomuunga Naibu Wake William Ruto wakimuasi hadharani.

Kumekuwa na minong’ono kwamba, Rais Kenyatta analenga kutumia ripoti hiyo kubadilisha katiba ili aendelee kuhudumu baada ya kipindi chake kukamilika 2022.

Mwishoni mwa mwaka 2019 mwandani wake, David Murathe ambaye alikuwa naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, alisema kwamba, katiba itakabadilishwa mwaka huu ili kumruhusu Rais kuendelea kuwa serikalini baada ya 2022.

Ni kupitia kuteua na kumjenga mrithi wake eneo la Mlima Kenya mwaka huu ambako kutafanya Wakenya kuamini hana nia ya kukwamilia mamlakani.

Akiwa kiongozi wa chama tawala cha Jubilee ambacho kimekubwa na mzozo wa ndani kwa ndani uliozua makundi mawili ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ mwaka 2019 Rais Kenyatta atakuwa na kazi ya kuhakikisha kwamba hakijasambaratika kitakapofanya uchaguzi wa maafisa Machi 2020.

Kuhakikisha umoja chamani, ni muhimu katika juhudi zake za kuachia Wakenya kumbukumbu iwapo atastaafu 2022 kwa sababu atawategemea wabunge kupitisha miswada ya serikali bungeni.

Aidha, wandani wa mshirika wake katika handisheki, Raila Odinga wanahisi kwamba huenda anatumia BBI kama chambo kuhakikisha kuna utulivu nchini na hatimaye ampige chenga uchaguzi mkuu ukikaribia na kukosa kutekeleza BBI.

Akiwa kiongozi wa nchi, Rais Kenyatta atakuwa na kibarua kuhakikisha utekelezaji wa BBI hautagawanya nchi zaidi iwapo kura ya maamuzi itafanyika.

Ikizingatiwa amekuwa akitofautiana na Naibu Wake William Ruto kuhusu handisheki, vita dhidi ya ufisadi na BBI, Rais Kenyatta atalazimika kuhakikishia Wakenya kuwa tofauti hizo hazitaathiri utendakazi wa serikali.