Mlinzi wa gavana aibiwa bastola katika mazishi ya Raila
PATASHIKA ilitokea baada ya mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga Jumapili, pale mlinzi mmoja wa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alipopokonywa bastola yake yenye risasi 15.
Kulingana na taarifa ambayo polisi walitoa Jumatatu, afisa huyo wa kikosi cha GSU pia alijeruhiwa alipokuwa aking’ang’ana na wahuni hao kuokoa silaha yake.
“Afisa huyo wa cheo cha konstebo ambaye wakati huu ni mlinzi wa Gavana wa Kakamega, alivamiwa na kunyang’anywa bunduki katika kisa hicho kilichotokea saa kumi na nusu jioni,” ikaeleza taarifa hiyo ya polisi.
Kisa hicho kilitokea baada ya kukamilika kwa Ibada ya Mazishi ya Odinga katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), mjini Bondo, Kaunti ya Siaya.
Afisa huyo, ambaye jina lake limebanwa, alikuwa pamoja maafisa wengine wanne na walikujwa akiondoka kutoka ibada hiyo kabla ya kunyang’anywa bunduki yake kwenye lango kuu la JOOUST.
“Alisema alipokuwa akipanda gari rasmi la Gavana, vijana waliokuwa wamemzingira Gavana walipokonya bunduki yake aina ya Jericho yenye risasi 15 na wakatoroka,” ikaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Kituo cha Polisi cha Bondo.
Juhudi za kuwakamata wahalifu hao ili kukomboa silaha hiyo hazikufaulu kutokana na ukubwa wa umati uliokuwa ukizua fujo.
“Juhudi za kukomboa bunduki hiyo zimeanzishwa,” ikasema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, watu kadhaa walipoteza mali yao katika sherehe hiyo ya kumwaga Bw Odinga aliyefariki mnamo Jumatano, Oktoba 15, 2025 nchini India alikokuwa akipokea matibabu.
Mwanasiasa huyo mashahuri alizikwa nyumba kwa babake, Jaramogi Oginga Odinga, Kang’o Ka Jaramogi, kijiji cha Nyamira, Bondo.