Habari

Moi alihakikisha timu zimefadhiliwa vilivyo

February 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

AYUMBA AYODI na JOHN ASHIHUNDU

MWANARIADHA jagina Kipchoge Keino na Waziri wa Michezo Amina Mohamed waliongoza wapenzi wa michezo nchini kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Kenya, Mzee Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne asubihi katika Nairobi Hospital.

Kadhalika, wakuu wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock) na wale wa Chama cha Riadha Kenya (AK) walituma salamu zao za pole kufuatia kifo hicho.

Keino ambaye alikuwa kwenye timu ya taifa iliyovuma katika Michezo ya Olimpiki za 1968 na 1972, akiwakilisha taifa katika mbio za mita 1,500 na mita 3,000 alimtaja marehemu kama mtu aliyependa michezo.

Mwanariadha huyo mstaafu alisema Mzee Moi alihakikisha wanamichezo wanapata mazingara mazuri ya kuwafanya wafaulu.

“Kwa kuthibitisha madai yangu, Moi alijenga Nyayo Stadium mnamo 1983, akajenga MISC, Kasarani mnamo 1987. Alihakikisha viwanja vingine kama Ruring’u mjini Nyeri na Moi Stadium, Kisumu vinawekwa katika hali nzuri ya kuandaa michezo mbalimbali,” alisema Keino.

Kipchoge anaeleza kuwa kujengwa kwa viwanja hivi kuliiwezesha Kenya kupiga hatua kubwa michezoni, mbali na kupata fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa, pamoja na kuimarisha vipaji vya wanamichezo nchini ambao walivuma katika ngazi ya kimataifa.

Hata hivyo, mkongwe huyo alishutumu viongozi waliofuata kwa kuzembea katika jukumu hilo, huku akimsifu marehemi Moi kwa kuhakikisha vyuo vyote vikuu vya UoN na Kenyatta vimepata vifaa vya kisasa alipokuwa mamlakani.

“Moi alihakikisha timu zetu za kushiriki Michezo ya Olimpiki, Michezo ya Madola na mashindano mengine makubwa zimefadhiliwa ipasavyo na kufanya vyema.”

Kadhalika, Kipchoge anamkumbuka marehemu kwa kutambua wanamichezo walioletea taifa sifa za kimataifa.

“Wakati wake, hatukuwa na shida za ukosefu wa pesa za kugharamia timu ya taifa,” akasema.

Kwa upande wake, waziri Amina alimkumbuka marehemu Moi kama kiongozi aliyejali zaidi maisha ya akina mama na watoto. Moi alipenda kusaidia watoto wetu kupata elimu bora, kwa kuhakikisha kuna madarasa yanayofaa, mbali na maziwa kwa watoto wa shule.

‘Natoa salamu zangu za pole kwa Seneta Gideon Moi, familia nzima ya marehemu na Wakenya kwa jumla,” alisema Amina.

Taarifa ya Nock ilimwomboleza Moi kama shabiki mkubwa wa michezo wakati wote tangu Kenya ipate uhuru hata kabla ya kutwaa mamlaka mnamo 1978 kuongoza taifa hadi 2002.

Aliisaidia Kenya kupata tiketi ya kuandaa Michezo ya Bara Afrika kwa mara ya kwanza mnamo 1987 ambapo timu ya soka ilitinga fainali ya michuano hiyo kabla ya kushindwa 1-0 na Misri.

Moi anakumbukwa kwa kuwa katika kikosi cha Bunge FC cha miaka ya sitini ambacho pia kiliwajumuisha marehemu Tom Mboya, Bruce MacKenzie, Robert Ouma miongoni mwa wengine.

Nayo kamati ya AK ilipendekeza Serikali ihakikishe miradi yote aliyoanzisha Moi imekamilika kwa heshima yake.