Moses Kuria: Tishio la kufunga Naivas linahatarisha ajira chache zilizopo
VIONGOZI mbalimbali wamejitokeza kuikashifu serikali ya Kaunti ya Nairobi kufuatia mvutano uliotokea Mei 14, 2025 wa tishio la kufunga kwa mojawapo ya tawi la duka la jumla la Naivas kwa tuhuma za kuuza ‘bidhaa zilizoharibika’.
Moses Kuria, mshauri mkuu wa Rais William Ruto kuhusu masuala ya kibiashara na uchumi, alikemea hatua hiyo huku akisema kuwa serikali ya kaunti haifai kufifisha juhudi za serikali za kuunda nafasi za ajira nchini.
“Hatutaunda nafasi za ajira kisha serikali ya kaunti inaamua kufunga duka kama vile Naivas na Carrefour bila kufuata sheria mwafaka. Hatua kama hiyo inawafukuza wawekezaji,” Bw Kuria alisema katika mtandao wak wa kijamii.
Kwa upande wake, mbunge wa Embakasi East, Babu Owino alisema kuwa, “Inasikitisha sana kuona ripoti za Gavana wa Kaunti ya Nairobi akiwatisha wamiliki wa biashara, ikiwa ni pamoja na tukio la hivi lililohusisha Duka la jumla la Naivas. Madai kuwa duka hilo linauza bidhaa zilizoharibika ni potovu na hayana msingi.”
Aliongeza kuwa hatua hiyo inaonyesha ufisadi uliokithiri katika kaunti ya Nairobi.
Kauli yao yanajiri kufuatia tukio la Jumatano Mei 14, 2024 ambapo Mwenyekiti wa kamati ya Afya, Maurice Ochieng pamoja na madiwani wengine walipotembelea Naivas tawi la Moi Avenue kufanya ukaguzi na kusema kuwa tawi hilo linafaa kufungwa kwa kuuza bidhaa zilizoharibika.
Baadaye, serikali ya Kaunti ya Nairobi kupitia afisa wa kaunti anayesimamia masuala ya afya Tom Nyakaba ilionekana kujitetea ikisema kuwa duka hilo halifai kufungwa kwani kuna ukaguzi mwingine uliofanywa siku iyo hiyo na kuonyesha kuwa kila kitu kiko sawa.
“Serikali ya Kaunti ya Nairobi ingependa kujulisha umma kuwa haikutoa agizo duka la jumla la Naivas lifungwe kama ilivyoripotiwa hapo awali wakati wa ukaguzi ulioongozwa na kamati ya kaunti inayosimamia sekta ya afya,” barua hiyo ilisoma.
“Baada ya ukaguzi huo, tumegundua kuwa masuala yalioibuliwa hayakufaa kufikia kwa hatua ya tawi la duka hilo kufungwa. Kulingana na matokeo hayo, serikali ya kaunti ya Nairobi imeamua duka hilo liendelee kutoa huduma huku barua hitajika zikikaguliwa katika ngazi ya juu.”