Habari

Moto katika mbuga ya wanyama ya Nairobi ulisababishwa na sigara – Waziri Miano

March 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori, Bi Rebecca Miano, amethibitisha kuwa moto ulioteketeza ekari 210 kati ya 28,000 katika mbuga ya Kitaifa ya Nairobi ulisababishwa na kipande cha sigara kilichotupwa karibu na hifadhi hiyo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Waziri Miano alisema moto huo, ambao ulizuka katika eneo la Athi Basin karibu na Kitengela, uliweza kuzimwa kwa mafanikio kupitia juhudi za mashirika mbalimbali.

“Huu ni msimu wa moto, unaoendelea kutoka Januari hadi Machi, ambapo hali ya ukame huongeza hatari ya moto porini. Kama mnavyoona, eneo lililoathirika ni sehemu ya mwisho ya hifadhi karibu na barabara. Inaonekana mtu aliyepita alitupa sigara iliyokuwa imewashwa, ikachoma nyasi kavu na kusababisha moto kuenea haraka,” alisema Waziri Miano.

Moto huo ulioanza mwendo wa saa kumi jioni ulidhibitiwa baadaye usiku, huku kikosi cha pamoja kikihusisha Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS), Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), timu za serikali za kaunti, mashirika ya usalama, na wanajamii wa eneo hilo.

Waziri Miano alisifu hatua ya haraka ya vikosi vya kukabiliana na moto, akisisitiza kuwa hakuna mnyama yeyote aliyeripotiwa kuathirika.

Waziri Miano akizungumzia kuhusu sehemu ya ardhi yenye ekari 210 iliyoteketea katika Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi. Picha: Fridah Okachi

“Licha ya moto huo kuteketeza eneo kubwa, hakuna vifo vya wanyamapori vilivyorekodiwa. Pia nataka kuwahakikishia wageni kuwa hifadhi inaendelea kufanya kazi, na shughuli za utalii, ikiwemo safari za kutazama wanyama, zinaendelea kama kawaida,” alisema.

“Nimejulishwa waziwazi kuwa hakuna mnyama aliyefariki kutokana na moto huu. Askari wa KWS, hasa wale wa kitengo cha ufuatiliaji wa faru, walijulishwa na wakajibu haraka kuhakikisha usalama wa wanyamapori kwenye hifadhi hii,” alifafanua.

Ingawa chini ya asilimia 1 ya ardhi yote ya hifadhi iliyoathiriwa, Waziri Miano alikiri kuwa hata uharibifu mdogo wa makazi ya wanyama unaweza kuwa na athari za mazingira.

“Kisayansi, kupotea kwa makazi ya wanyamapori, hata kidogo, kunaweza kuathiri bayoanuwai. Lakini tuna bahati kwamba tukio hili lilizimwa haraka na halikusababisha janga kubwa zaidi la mazingira.”

Alieleza pia kuwa kumekuwa na matukio mengine ya moto porini katika maeneo ya hifadhi nchini, ikiwemo moto katika mfumo wa ikolojia wa Aberdare, Hifadhi ya Taifa ya Ruma, na Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa Kusini huko Kaunti ya Marsabit katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Alihusisha ongezeko hilo na shughuli za binadamu, hali ya hewa, na visa vya uchomaji wa makusudi, akiwataka wananchi kuwa waangalifu hasa wakati wa msimu wa kiangazi.