Habari

Moto: Zaidi ya familia 100 zapoteza makazi yao Mukuru-Kayaba

Na SAMMY KIMATU December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMIA waliachwa bila makazi eneo la Mukuru-Kayaba, South B katika Kaunti Ndogo ya Starehe, baada ya moto kuzuka na kuteketeza nyumba zao.

Hii imezua wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya moto katika mitaa ya mabanda Nairobi.
Moto huo ulioanza Jumapili usiku katika eneo la Tulanga, na kuenea kwa kasi kabla ya wakazi na wahisani kujitolea kuuzima.
Baadaye, polisi, maafisa wa utawala wa eneo hilo pamoja na kikosi cha zimamoto cha Kaunti ya Nairobi kutoka Kangundo Road walifika kwenye eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Makadara, Bi Judith Nyongesa, alithibitisha kwamba uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha moto huo.
“Tumetuma maafisa eneo la tukio kukusanya taarifa za kina na kubaini kilichosababisha moto,” aliambia Taifa Dijitali.
Benard Munyao, mkazi mwenye umri wa miaka 60 na shahidi katika tukio hilo, alisema moto ulisambaa kwa kasi kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma.
“Ulitoka kwenye nyumba moja ambayo mwenyeji aliwacha mshumaa ukiwaka,” alisema.
Bi Penninah Mutuku, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 40, alisema aliponea kwa tabu pamoja na watoto wake wawili wakati moto ulipoelekea nyumbani kwake.
“Niliweza kuwaokoa watoto wangu wawili,” alisema.

Familia yake sasa ni miongoni mwa kadhaa zilizolazimika kulala nje, baadhi kwenye barabara na maeneo ya wazi wakisubiri msaada.