Habari

Mpango wa harusi waishia kuwa ya mazishi

Na MERCY KOSKEI November 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HUZUNI imetanda katika familia ya Brian Rotich mwenye umri wa miaka 24 ambaye amepoteza mchumba wake wiki chache tu kabla ya harusi yao.

Wawili hao, Rotich na mwendazake Dorcas Cherono, 20, walipanga kufanya harusi Desemba 18, 2025.

Hata hivyo, mpango huo wa furaha sasa umegeuka kuwa huzuni baada ya Bi Cherono kuzirai na kufa akiongoza ibada kwa nyimbo za sifa katika kanisa la Kipsege Church of God Kaunti ya Kericho mnamo Novemba 15.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Londiani ambako madaktari walitangaza kuwa amefariki.

Wawili hao walifaa kufunga ndoa katika Kanisa la Sayunist Church of God Rongai.

Kulingana na Bw Rotich, alifahamishwa kuhusu mkasa huo mnamo Novemba 16 kupitia kwa mzee wa kanisa lake aliyemtembelea nyumbani kwake akiandamana na viongozi wengine wa kanisa na wazee wa kijiji.

“Nilidhani walikuwa wamekuja kuuliza kuhusu maandalizi ya harusi, lakini nyuso zao zilieleza habari tofauti. Baada ya kupata ujasiri, walinieleza habari kwamba Cherono ameaga,” alisema.

Rotich aliambiwa kuwa asubuhi ya siku hiyo ya mkasa, Cherono aliamka mapema akiwa mchangamfu na mwenye furaha tele, na kufurahia kuongoza ibada hiyo.

Akiwa njiani, alisimama karibu na nyumba ya kaka yake lakini alipomkuta shemeji yake bado hajajitayarisha, aliendelea na safari peke yake.
Alipofika kanisani, alikuta ibada ikikaribia kuanza.

Alikusanya vijana fulani nje, akiwatia moyo kubaki imara katika imani, kumtumikia Mungu na kamwe wasikose kanisani. Hata aliwakumbusha kuhusu harusi yao.

Kurudi ndani ya kanisa, Cherono alichukua kipaza sauti na kuanza kuimba.

“Alikuwa akiongoza kipindi cha kusifu wakati ghafla alishika kifua chake, akayumbayumba na kuzimia,” Rotich alisimulia. “Hofu ilitanda kanisani.

Walimkimbiza nje na kumpatia huduma ya kwanza. Alilalamika kuhusu maumivu ya kifua na akaomba maji. Alimwambia mama yake kwamba anakufa.”