Mpango wa kumng'oa Naibu Rais wakanganya wapinzani
Na JUSTUS OCHIENG
WAFUASI wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamechanganyikiwa kuhusiana na madai ya Seneta wa Siaya James Orengo kwamba kuna mipango ya kumng’oa Naibu Rais William Ruto kwa kupitia hoja bungeni
Ingawa wanasiasa walioko katika kambi ya Uhuru na Raila wanakubaliana kwamba azma ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022 imeathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake, hawajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo anafaa kuondolewa afisini au la.
Hii ndio maana tangu Bw Orengo afichue mipango hiyo zaidi ya wiki mmoja iliyopita, seneta huyo wa Siaya hajasema lolote kuhusu suala hilo sawa na wafuasi wengine wa Bw Odinga.
Lakini kwa upande mwingine, wafuasi wa Rais Kenyatta wameendeleza shinikizo za kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu, bila kusema lolote kuhusu hoja ya kumng’oa mamlakani.
Wabunge hao watetezi wa Rais wanasema kuwa hoja kama hiyo inaweza kusababisha “taharuki” nchini na kuyumbisha ajenda za maendeleo za serikali.
Na wadadisi wanashikilia kuwa miito ya kumng’oa mamlakani Dkt Ruto itamfaidi kisiasa na kupelekea Wakenya wengi kuhisi kuwa ananyanyaswa kimakusudi.
Alhamisi, naibu kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata aliambia ‘Taifa Leo’ kwamba hawafahamu lolote kuhusu mipango ya kuwasilishwa kwa hoja kama hiyo, zaidi ya wiki mmoja baada ya madai ya Orengo.
“Sina habari kuhusu suala hilo. Hoja hiyo ilikuwa iwasilishwe na Orengo hivyo tusubiri. Mimi ni shabiki sugu wa handisheki lakini sidhani kama hatua kama hiyo itafaa wakati huu,” Bw Kang’ata akasema.
Kulingangana na seneta huyo wa Murang’a, Naibu Rais anaweza kutumia suala hilo la kuondolewa mamlakani kujiongozea umaarufu miongoni mwa wananchi.
“Napendekeza kwamba tushughulikie masuala mengine wala sio hili. Binafsi, licha ya kuwa mfuasi wa handisheki sidhani ikiwa ninaweza kuunga mkono mpango kama huo. Utaleta taharuki nchini,” akaongeza Bw Kang’ata.
Naye Mwenyekiti wa ODM John Mbadi hakuthibitisha ua kukana kufahamu kuhusu hoja hiyo ila akasema kuwa lengo kuu la Orengo ni kumtaka Dkt Ruto awajibike kwa Wakenya.
“Kuhusu hoja hiyo, kile ninachoelewa ni kwamba Orengo anamtaka Ruto awajibike kwa Wakenya na akome kumkanganya Rais hadharani kila mara.
Wachanganuzi wa kisiasa sawa na wafuasi wa Rais Kenyatta, pia wanaonya dhidi ya mipango ya kumng’oa mamlakani Dkt Ruto, wakisema itasababisha madhara mengi kuliko faida.
Ingawa wanasema kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaweza kutumia vyombo vya dola kumlemea Dkt Ruto, wanaonya kuwa hatua kama hiyo itamfaidi Naibu Rais kisiasa, ikizingatiwa kuwa amekuwa akilalamika kwamba anahujumiwa na maafisa fulani serikalini.
“Uhuru na Raila watapata idadi ya wabunge kuunga mkono hoja kama hiyo. Lakini swali ni je, hatua kama hiyo itasababisha athari zipi za kisiasa?” Herman Manyora akauliza.
Akaongeza: “Uhuru anaweza kupata wabunge 233 kuunga mkono hoja hiyo. Lakini sidhani kama ni hatua ambayo itawafaa Uhuru na Raila kisiasa. Atakayefaidi ni Dkt Ruto.”
Bw Javs Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na kimaongozi, anasema kuwa hatua ya kumwondoa mamlakani Bw Ruto, kimsingi, itaonyesha kuwa “Rais Kenyatta ambaye ni bosi wake hana imani naye.”
“Mchakato kama huo ni wa kisiasa na ambao hufanikishwa kwa kuzingatia mkondo wa sheria. Suala la ukiukaji wa Katiba halijakuwa msukumo wa kumfuta kazi afisa wa cheo cha Naibu Rais katika mataifa yanayozingatia mfumo wa uongozi wa kidemokrasia,” anasema.
Bw Bigambo anaongeza: “Kwa hivyo mipango ya kuwaondoa mamlakani afisa wa hadhi ya Dkt Ruto huwa ni wenye misukumo ya kisiasa na haja ya kulipiza kisasi. Na kwa mujibu wa kipengee cha 150 cha Katiba ikisomwa pamoja na vipengee 144 na 145, kimsingi hatua ya kumwondoa mamlakani Dkt Ruto itaashiria kuwa wanaodhibiti mamlaka serikalini wamekosa imani naye.”
Hata hivyo, changamoto kuu katika ufanikishaji wa mpango wa kumwondoa Ruto mamlakani ni kupatikana kwa idadi tosha ya wajumbe katika mabunge yote mawili kuunga mkono hoja kama hiyo.
“Ikiwa kutahitajika zaidi ya wajumbe 230 katika bunge la kitaifa na maseneta 45 kupitisha hoja kama hiyo, basi itakuwa vigumu kumwondoa mamlakani Dkt Ruto au hata Rais Kenyatta,” Bw Bigambo akasema.
Mchanganuzi huyo, sawa na Bw Manyora, anasema kuwa Rais Kenyatta anaweza kutumia nguvu na kisiasa na kifedha kumwondoa mamlakani Dkt Ruto lakini “huenda hatua kama hivyo ikamgharimu Rais kisiasa.”
Lakini Bw Richard Atemba ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa kutoka kaunti ya Kisii, hata hivyo anasema kuwa idadi ya wabunge waliojitokeza kumtetea Dkt Ruto wiki jana, ni ithibati kuwa hoja ya kumwondoa mamlakani itafeli.
Hata hivyo, Bw Manyora anapuuzilia mbali kauli hiyo.
“Kwa kuzingatia idadi ya wabunge kutoka kambi hiyo mbili waliohutubia wanahabari juzi Jumatano, itakuwa kosa kumdai kuwa Dkt Ruto anaweza kuondolewa kwa urahisi,” anasema Bw Atemba.
Anasema kuwa hatua hiyo haina uhusiano wowote na maadili ya Naibu Rais bali linahusu siasa za urithi mnamo mwaka wa 2022.
“Hili suala la hoja ya kumwondoa Ruto mamlakani ni sehemu ya mikakati ya siasa za 2022. Hatua kama hiyo bila shaka itavuruga mchakato wa BBI na kuigawanya nchi hata zaidi,” akasema.
Lakini mdadisi wa masuala ya kisiasa Samuel Owida anasema kuwa ikiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga watawaagiza “wandani wao wamfute kazi Naibu Rais, bila shaka hoja hiyo itapita.