Habari

Mradi wa Galana Kulalu ‘kufufuliwa kwa nguvu’

February 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JULIUS SIGEI

MRADI wa unyunyiziaji mashamba maji wa Galana-Kulalu utafufuliwa na mashamba mengine kuzinduliwa, balozi wa Israel nchini Oded Joseph amesema.

Alisema mradi huo unaogharimu mabilioni ya fedha ni kiungo muhimu katika uhusiano kati ya Kenya na Israel wala haufai kusitishwa kwa sababu utaleta mabadiliko makubwa kiuchumi nchini Kenya.

Kufikia sasa, zaidi ya Sh6 bilioni zimetumika katika mradi huo wa kilimo kupitia unyunyiziaji.

Mnamo Agosti 2014 Bodi ya Kitaifa ya Unyunyiziaji (NIB) ilitia saini kandarasi ya Sh14.5 bilioni na kampuni ya Green Arava Ltd kuanzisha kilimo cha mahindi katika eneo la Galana-Kulalu lililoko katika kaunti za Kilifi na Tana River.

Kufikia Machi 2018 ni eneo la ekari 5,000 pekee kati ya ekari milioni moja zilizolengwa, ambalo lilikuwa limepandwa mahindi. Na maafisa wa serikali waliliambia bunge kwamba eneo hilo lilizalisha magunia 22,000 pekee ya mahindi, ya thamani ya Sh35.2 milioni.

Mwaka 2019 kampuni ya Green Arava ilidai kuwa Sh1 bilioni, lakini usimamizi wa bodi hiyo ulishikilia kuwa kiasi hicho cha fedha ni Sh200 milioni pekee.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, aliungama kuwa mradi huo ulivurugwa na ufisadi. Alielekeza kidole cha lawama kwa watu ambao hakuwataja kwa kupandisha gharama kupita kiasi.

Lakini Balozi Joseph alisema kuna muafaka miongoni mwa wadau ambao amezungumza nao wamejitolea kufufua mradi huu kwa manufaa ya taifa.

“Tunaendeleza juhudi za kuwaleta pamoja wadau wote ili tufanye uamuzi mzuri wa kufufua mradi wa Galana-Kulalu,” akasema.

Alisema mbali na mradi huo, vituo vingine viwili vitaanzishwa ambako wakulima watapata usaidizi kila “mchana na usiku.

“Chini ya mpango huo, wakulima watapewa mafunzo kuhusu teknolojia ya kilimo kutoka Israel, katika mashamba maalum kwa kipindi cha miaka mitano au saba,” Bw Joseph akasema.

Balozi huyo alisema kufufuliwa kwa mradi huo kutaendeleza ajenda ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini.

Hata hivyo, Joseph alidinda kufichua changamoto ambazo zilipelekea mradi huo kupata sifa mbaya hadi ukasitishwa.

Hata hivyo, alisema ili mradi huo ufanikiwe mahitaji mengine muhimu kama vile barabara, maji na umeme sharti yawepo.

“Shughuli za kilimo haziwezi kufanikiwa bila barabara ya kupeleka mazao sokoni au kupelekea mitambo shambani.

Umeme na maji yanapaswa kuunganishwa ili maeneo kama hayo yaweze kuwavutia wawekezaji wengine pamoja na watalii,” akasema.