Habari

Msahau makosa ya Moi, ashauri Raila

February 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga amewataka Wakenya kusahau makosa ya Rais mstaafu Daniel Moi – ambaye alifariki Jumanne wiki jana – na badala yake watilie maanani mazuri aliyotimiza wakati wa utawala wake.

Akiongea Jumanne wakati wa ibada ya kitaifa ya kumuenzi Moi katika uwanja wa michezo ya Nyayo, Nairobi, amesema kama binadamu yeyote yule, Mzee Moi alifanya makosa kadha wakati wa utawala wake.

“Alifanya mengi mazuri lakini kama binadamu aliteleza hapa na pale lakini akaomba msamaha. Binafsi nilikuwa mwathirika wa hayo lakini baadaye tukasameheana na kushirikiana kuunda katiba mpya,” amesema Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa ODM amemtaja kiongozi huyo kama mpiganiaji mashuhuri wa uhuru wa Kenya kabla ya kupanda ngazi hadi kuwa makamu wa Rais na hatimaye Rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya.

“Alitwaa mamlaka ya nchi wakati ambapo taifa hili lilikuwa likipitia mabadiliko makubwa katika nyanja za uongozi,” Bw Odinga amesema.

Miongoni mwa mambo mazuri ambayo amesema Moi alifanya akiwa Rais ni kuanzisha mpango wa Elimu kwa Wote nchini, mpango wa kutoa maziwa ya bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na kupalilia umoja miongoni mwa Wakenya.

Bw Odinga ambaye pia ni Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi ametumia fursa hiyo kwa niaba ya familia ya Jaramogi Oginga Odinga kutuma salamu za pole kwa familia ya Mzee Moi.

“Tungependa kuendeleza mazuri ambayo Rais Moi alifanya na kuyaweka katika mchakato wa maridhiano (BBI),” amesema.