Msalimie Orengo yuko hapa, Raila amkumbusha Uhuru
Na CHARLES WASONGA
WAGENI mashuhuri waliohudhuria sherehe za Madaraka Dei Jumamosi katika Uwanja wa Michezo wa Narok walichangamshwa na hatua ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kumkumbusha Rais Uhuru Kenyatta kumsalimia Seneta wa Siaya James Orengo.
Rais alikuwa amewasili uwanjani humo mwendo wa saa tano mchana na kuwasalimia watu mashuhuri waliokuwa wamefika, wakiwemo Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale, Gavana wa Narok Samuel Tunai na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.
Lakini kabla ya kiongozi wa taifa kuketi, Bw Odina alimgusa begani kumkumbusha kuwa alikuwa amesahau kumsalimia Bw Orengo ambaye alikuwa ameketi katika safu ya pili.
Kitendo hicho kiliibua kicheko kutoka kwa viongozi hao na wananchi ambao walikuwa wamehudhuria sherehe hizo.
Rais Kenyatta alirejea taratibu katika kiti chake.
Usalama waimarishwa
Wakati uo huo, usalama ulikuwa umeimarishwa zaidi mjini Narok huku vikosi mbalimbali vya walinda usalama wakishika doria.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 22 alikamatwa asubuhi akijaribu kuingia katika uwanja huo kwa madai ya kuwa mfuasi wa kundi la kigaidi.
Adan Galhai maarufu kama, Urisha Galhai, alikamatwa kwa kujifanya kama afisa wa usalama.
“Alikuwa akijaribu kuingia katika uwanja wa michezo Ijumaa. Tulipomsaka, tuligundua kuwa alikuwa na vitambulisho viwili. Na tulipotaka kujua sababu ya yeye kuwa na vitambulisho hivyo akajaribu kutoroka na ndipo tukamkamata,” taarifa ya idara ya polisi ikasema.