Msemaji wa polisi asema anasikitikia maafa nyakati za maandamano
MSEMAJI wa Polisi Michael Michiri Nyaga amealezea matumaini kuwa maridhiano yatafikiwa kati serikali na vijana wa kizazi cha kisasa Gen Z.
Kwenye mohajiano ya kipekee na Taifa Leo afisini mwake, Bw Nyaga alisema yeye pia anahitaji machungu yanayowakumba vijana hao kwani watoto wake pia ni wa kizazi hicho.
Afisa huyo alieleza kuwa tangu mwaka jana mwanawe wa kiume anayesomea katika chuo kikuu kimoja nchini amekuwa akizungumzia maandamano, ukatili wa polisi na maafisa yaliyosababishwa na watu wenye wajibu wa kuwalinda.
“Mwana wangu mwenye wa miaka 20 ni mwanafunzi chuoni. Endapo ataamua kujiunga na maandamano au la hilo ni chaguo lake, sitamwaamulia. Kwa hivyo, wanahurumia wale ambao wamepoteza watoto wao kwa sababu mimi pia ni mzazi kwanza na inaniuma maisha yanapokatizwa kwa njia yoyote ile,” Bw Nyaga akaambia Taifa Leo.
“Sisi kama maafisa wa polisi, kwa kujadiliana kivyetu, hatuwezi kujifanya kwamba kila kitu ki shwari na sharti kwanza tutambue changamoto zinazowakumba vijana,” akaongeza.
Msemaji huyo wa polisi alisema kuwa humo humo ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) maafisa wanahimizwa kutambua kwamba “hizo siyo nyakati za kawaida.”
“Tunapata mafunzo fulani na tunapaswa kuyatumia ili kuboresha utendakazi wetu ili uafikiane na matakwa ya vijana,” akaeleza Bw Nyaga.
Msemaji huyo wa polisi alifichua kuwa zaidi ya maafisa 300 wa polisi walijeruhiwa vibaya wakati wa maandamano ya Juni 25 ya kuwakumbuka vijana 60 waliouawa Juni 25, 2024 wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.
“Hizi hazikuwa majeraha ya kimwili tu. Wengi wanaumiza na machungu ya kisaikolojia. Polisi anaporushiwa jiwe anapatwa na machungu maradufu,” akaeleza Bw Muchiri.
Alielezea kuhusu video iliyosambaa mitandaoni ya afisa mmoja wa kike kwa jina Emily akishambuliwa na waandamanaji kama kielelezo ya masaibu na hatari zinazowakumba polisi nyakati za maandamano.
“Afisa huyo aliponea kifo kwa tundu la sindano. Lakini kwenye video hiyo kijana mmoja anaonekana akimkinga asiumizwe zaidi. Tukio hilo linatoa maana kubwa kuhusu yale yanayowakumba maafisa wetu,” akaeleza kwenye mahojiano ya kipekee.
Bw Muchiri aliyeongoza operesheni za kupambana na waandamanaji eneo la Kikuyu mnamo Juni 2024 alisema yale ambayo walipitia yameacha majeraha yasiyopona maishani mwao.