Mshukiwa aliyeshtakiwa na mbunge wa zamani, ajiwasilisha kortini
MKURUGENZI wa Kampuni ya Shaba Trustees Brian Kiptoo Kiplagat ambaye ameshtakiwa pamoja na Mbunge wa zamani wa Baringo ya Kati Sammy Mwaita kuhusu ulaghai wa shamba lenye thamani ya Sh300 milioni, Jumanne alijiwasilisha kortini.
Kiplagat alijiwasilisha kortini na kukanusha mashtaka matatu ya kula njama za kuwalaghai Rose Njoki Kang’au na Mucugu Wagatharia shamba hilo linalopatikana Nairobi West.
Alipojisalamisha mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani Benmark Ekhubi Kiptoo, alikana kuwalaghai Bi Njoki na Bi Mucugu huku akishikilia a shamba hilo ni lake na alipewa na serikali miaka 24 iliyopita.
Kiptoo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni ama pesa tasilimu Sh1milioni moja naye Mwaita anayekabiliwa na mashtaka sita, yuko nje kwa dhamana ya Sh10 milioni ama Sh2milioni pesa tasilimu.
Mwaita ameshtakiwa kutumia mamlaka yake vibaya kuandikisha mashamba ya Bi Njoki na BI Mucugu kwa jina la Shaba Trustees kitendo alichokitekeleza mnamo Machi 30, 2001 wakati huo akiwa kamishina wa ardhi.
Bw Kiplagat alikuwa akifika kortini mara ya kwanza mnamo Jumanne baada ya Hakimu Ekhubi kutoa agizo afanye hivyo mnamo Jumatatu.
Kesi hiyo itasikizwa mnamo Septemba 10.