Habari

Mshukiwa wa Al-Shabaab aliyepanga utekaji Mandera alituma ombi la kupata kitambulisho

Na MANASE OTSIALO February 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WASHUKIWA wawili wanaohusishwa na njama ya kuteka nyara wafanyakazi wawili wa kigeni kwenye mradi wa serikali ya Kaunti ya Mandera Mashariki walikamatwa na maafisa wa Kupambana na Ugaidi (ATPU) katika Kituo cha Polisi cha Mandera.

Kulingana na Afisa wa Upelelezi wa Jinai Kaunti ya Mandera (CCIO), Bw Pius Gitari, Isaack Abdi Mohamed almaarufu Kharan Abdi Hassan na Noor Yakub Ali, wanashukiwa kupanga shughuli za kigaidi katika kaunti hiyo.

“Tunawazuilia kwa kuhusishwa na kupanga shughuli za kigaidi za Al-Shabaab huko Mandera. Uchunguzi unaendelea kabla ya kuwafikisha mahakamani,” alisema Bw Gitari.

Ripoti kutoka Idara ya usalama inaonyesha kuwa, Bw Abdi aliingia nchini kutoka eneo la El-Ade, Somalia hivi karibuni na kupata kitambulisho kumruhusu kusafiri kwa uhuru.

Ilidaiwa Bw Abdi, alimlipa mkazi wa Mandera Sh100,000, kuwezesha utekaji nyara wa wafanyakazi raia wa China wanaohusika na mradi wa maji taka karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Bw Gitari alisema kuwa kukamatwa kwa washukiwa hao kulifanikishwa na taarifa za kijasusi zilizotolewa na raia hivi karibuni.

Walibainisha kuwa washukiwa hao, walipanga kuwapeleka mateka wao hadi El-Ade kwa gharama ya Sh300,000.

Kukamatwa kwa wawili hao, Ijumaa asubuhi, kunajiri wakati ambapo usalama umeimarishwa Mandera, wiki chache baada ya machifu watano kutekwa nyara na kupelekwa Somalia.