Habari

Mshukiwa wa tatu mauaji ya mwanamke na wanawe wawili akamatwa Nanyuki

November 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOSEPH WANGUI

MAAFISA wa polisi wamemkamata mshukiwa wa tatu wa mauaji ya mwanamke Joyce Syombua na watoto wake wawili Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Mshukiwa huyo mtaalamu wa uunganishaji umeme na vifaa vya kielekroniki Peter Maina Mwangi, alikamatwa Alhamisi jioni na wapelelezi wa kutoka kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa kutoka makao makuu Nairobi.

Anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiganjo, Nyeri kusubiri uchunguzi kufanywa.

Kwenye hati ya kiapo Ijumaa  katika mahakamani ya Nyeri, kiongozi wa mashtaka Bi Martha Ndung’u alisema ni mshukiwa kwa sababu alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na mshukiwa mkuu ambaye ni Peter Mugure; mume wa mwendazake pamoja na watoto wawili.

Mahakama iliombwa azuiliwe siku 14 uchunguzi ukamilike.

 

“Mwangi anashukiwa kuhusika kupanga, kutekeleza na hata kuizika miili ya wendazao,” amesema afisa mchunguzi wa mauaji ya kinyumbani Reuben Mwaniki katika hati ya kiapo aliyoipata hakimu mkuu Wendy Kagendo.

Syombua alifariki akiwa na umri wa miaka 31, pamoja na wanawe Shanice Maua aliyekuwa na umri wa miaka 10, na Prince Michael aliyekuwa na umri wa miaka mitano ambao miili yao ilipatikana imezikwa katika kaburi la kimo kifupi katika makaburi ya Nanyuki mjini.

Peter Mwaura Mugure aliyekuwa na cheo cha Meja katika kambi ya Laikipia Air Base tayari alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkuu Lucy Mutai.

Ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji hayo.

Mshukiwa mwingine ni Collins Pamba.