Msisumbue rais, tengeni pesa za maendeleo katika bajeti, Wetang’ula aambia Wabunge
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amewataka Wabunge kutenga fedha za kutosha kwa miradi ya maendeleo badala ya kuomba Rais William Ruto kuitekeleza katika maeneo yao.
Bw Wetang’ula aliwakumbusha Wabunge na kusisitiza kuwa maendeleo yanaweza kufanikishwa tu kwa kutenga fedha za kutosha kwa miradi husika.
“Ugavi wa rasilimali kwa miradi muhimu ya miundombinu ni jukumu la Bunge, si la Serikali Kuu. Ikiwa mnataka miradi ya maendeleo katika maeneo yenu, hakikisheni mnashiriki kikamilifu katika mchakato wa bajeti kwa kutenga fedha kwa miradi hiyo,” alisema Wetang’ula.
Spika Wetang’ula alitoa matamshi hayo katika hafla ya maombi yaliyofanyika katika Shule ya Upili ya Cheptais, Kaunti ya Bungoma ambayo Rais Ruto alihudhuria.
“Nimekuwa nikiwasikia Wabunge wakiomba miradi ya maendeleo kutoka kwa rais. Hata hivyo, nawakumbusha kwamba bajeti haitengwi Ikulu bali Bungeni. Ili kuhakikisha maeneo yenu yanapata miradi ya maendeleo, lazima mtenge fedha kwa utekelezaji wake katika bajeti,” Bw Wetang’ula alisisitiza.
Wakati huo huo, Spika Wetang’ula aliwahimiza Wabunge kutomweka rais katika hali ngumu kwa kushinikiza miradi ya maendeleo ambayo haijatengewa fedha katika bajeti.
“Wabunge wote mnaotaka miradi kama barabara, maji, na huduma za afya, hakikisheni mnaposhiriki katika mchakato wa bajeti mnatenga fedha kwa maendeleo,” aliongeza.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kaunti, akiwemo Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, na Waziri wa Afya, Deborah Mulongo.
Katibu Harry Kimutai na Juma Mukhwana pia walihudhuria pia, sawa na Gavana wa Bungoma Kenneth Makelo Lusaka, Maseneta David Wafula Wakoli (Bungoma) na Allan Chesang (Trans Nzoia) na Mbunge, Fred Kapondi wa Mlima Elgon