HabariSiasa

Mswada wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka kuliko Rais wapendekezwa

February 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY KILALO

Kwa ufupi:

  • Mswada unapendekeza Waziri Mkuu ambaye atakuwa mkuu wa serikali, atakayewateua na kuwafuta mawaziri, makatibu, mwanasheria mkuu na mabalozi
  • Seneta Mutula Kilonzo amepinga mswada huo akielezea kuwa iwapo kuna nia yoyote ya kubadilisha Katiba, lazima vipengee vyote viangaziwe 
  • Rais lazima awe na umri usiopungua miaka 50
  • Mswada unawataka mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge
  • Waziri mkuu ataweza kuondoka ama kujiuzulu iwapo kutakuwa na kura ya kutokuwa na imani naye
  • Unataka kuwepo na afisi ya kiongozi wa upinzani. Waziri Mkuu atakuwa na mamlaka ya kumteua Mkuu wa Mashtaka ya Umma

WADHIFA wa Waziri Mkuu utarudi katika utawala wa Kenya iwapo Kielelezo cha Mswada mpya uliodhaminiwa na Mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket (KANU) utapitishwa.

Mswada huo unapendekeza Waziri Mkuu ambaye atakuwa mkuu wa serikali na mwenye mamlaka ya kuwateua na kuwafuta mawaziri, makatibu, mwanasheria mkuu na hata mabalozi.

Wadhifa wa Rais utasalia lakini hatakuwa na mamlaka. Pia hatachaguliwa na wananchi bali na Bunge.

Kiongozi wa NASA Raila Odinga alishikilia nafasi ya Waziri Mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 uliokumbwa na ghasia. Nafasi hiyo iliundwa wakati huo kujaribu kutuliza joto la kisiasa kwa kuunda serikali ya muungano. Manaibu wake wakati huo walikuwa Musalia Mudavadi na Uhuru Kenyatta (rais wa sasa).

Mswada huo wa Bw Kamket unapendekeza kuwepo kwa manaibu wawili wa Waziri Mkuu.

Katika harakati za uchaguzi wa 2017, na hata baada ya utata kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais, suala la kuwepo kwa nafasi ya waziri mkuu pamoja na nafasi ya kiongozi wa upinzani limekuwa likichipuka, baadhi ya wanaopendekeza wakisema kuwa ni mojawapo ya suluhisho la kutatua mivutano ya kisiasa nchini.

Mbunge wa Tiaty, William Kassait Kamket. Picha/ Maktaba

Hata hivyo, Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo amepinga mswada huo akielezea kuwa iwapo kuna nia yoyote ya kubadilisha Katiba, lazima vipengee vyote viangaziwe na sio vya nyadhifa za uongozi pekee.

“Ikiwa wanataka hilo, basi kila kitu kwa Katiba kibadilishwe. Kwa sasa naona ni hali ya kujitafutia umaarufu tu wa kisiasa,” alisema katika mahojiano na Taifa Leo.

Bw Kamket anapendekeza katika mswada kuwa Rais achaguliwe na wabunge, asiwe na mamlaka isipokuwa kuwa ishara ya umoja wa kitaifa, na hafai kushikilia nafasi yoyote ya kuchaguliwa ama katika chama cha kisiasa.

“Rais atachaguliwa katika kikao cha pamoja cha Bunge ambacho kitaandaliwa Alhamisi ya kwanza ya kila mwaka wa saba ama kulingana na hali nyingine zilizopo kikatiba,” mswada huo wa Marekebisho ya Katiba 2017 unaeleza.

 

Umri wa rais

Rais huyo lazima pia awe na umri usiopungua miaka 50.

Kwa sasa, mbunge huyo atatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bajeti na Makadirio kutetea mapendekezo yake, hasa jinsi itakavyoathiri matumizi ya fedha za umma.

Baada ya kuwasilishwa bungeni, mswada huo utaelekezwa kwa kamati husika, kabla ya umma kushirikishwa kutoa mapendekezo yake katika muda wa siku 90. Mswada huo unawataka mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge.

Waziri mkuu kulingana na mswada huo ataweza kuondoka ama kujiuzulu iwapo kutakuwa na kura ya kutokuwa na imani naye ama serikali yake, hatua ambayo italihitaji bunge kufanya uchaguzi upya.

 

Kiongozi wa upinzani

Mswada huo unataka kuwepo na afisi ya kiongozi wa upinzani. Pia unapendekeza uchaguzi wa madiwani na magavana kuwa Jumanne ya pili ya Desemba kila mwaka wa tano.

Waziri Mkuu vile vile atakuwa na mamlaka ya kumteua Mkuu wa Mashtaka ya Umma baada ya kuidhinishwa na bunge.

Mbali na hivyo, pia unapendekeza mabadiliko katika uteuzi wa maseneta, na kutaka kuwa idadi iongezeke kutoka 47 wanaochaguliwa hadi 94. Kulingana naye, maseneta hao 94, mmoja wa kike na kiume, watawakilisha kila kaunti, na kuchaguliwa na Bunge la Kaunti.

Pia kutakuwa na wengine sita watakaoteuliwa kuwakilisha vijana na wenye ulemavu.