Mtu mwingine aliyepanda kikingi cha stima apigwa na umeme akafariki
POLISI mjini Nyamache, eneobunge la Bobasi Kaunti ya Kisii wameanzisha uchunguzi wa kifo cha mwanamume mmoja aliyepigwa na nguvu za umeme katika soko la Nyangusu.
Tuko hilo la kuatua moyo, lilitokea Jumanne mchana katika kituo hicho kilichoko kwenye mpaka wa kaunti za Kisii na Narok.
Kwa mujibu wa waendeshaji bodaboda walioshuhudia kisa hicho, walimwona marehemu aliyefahamika kama Julius Mbarage akipanda nguzo moja ya umeme karibu na kibanda chao lakini hawakushughulika kumzuia kwa kuwa waliamini alijua alichodhamira kufanya.
“Tulimuona saa sita hivi za mchana akipanda nguzo moja ya umeme iliyo karibu na banda letu. Kwa siku kadhaa sasa, tumekuwa tukipata milipuko kutoka kwa transfoma iliyo karibu na eneo letu na tulipomuona akipanda, tulidhani anaenda kurekebisha hali hiyo. Kwa bahati mbaya, alipigwa na umeme na kupoteza maisha papo hapo. Alirushwa kwa nyanya zingine na kukaushwa mara moja. Mwili wake ulisalia hewani hadi pale polisi na maafisa wa kampuni ya Kenya Power walipowasili kuuondoa,” Alex Ayuka, mwendeshaji wa bodaboda eneo hilo alisema.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyamache Kipkemoi Kipkulei alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa kisa hicho kimechukuliwa na Maafisa wa Kitengo cha Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI).

“Tumeanza kuchunguza kisa hicho. Tunashuku sana kuwa huenda marehemu alipanda nguzo ili kuunganishwa umeme kwa njia haramu aliponaswa na umeme kwa bahati mbaya. Ningependa kuchukua fursa hii kutuma rambirambi zangu kwa familia iliyoathiriwa,” Bw Kipkulei alisema huku akiwataka wananchi kuwahusisha wafanyakazi wa Kenya Power kila mara wanapokuwa na masuala ya umeme.
Ajali hiyo ya umeme ya Nyangusu inajiri siku moja tu baada ya mwanamume mwingine, Steve Ogero, 18, kupigwa na umeme kwa njia sawa na hiyo Jumatatu katika kijiji cha Iyabe eneobunge la Bonchari.
Kijana huyo alisemekana kupanda nguzo iliyo na umeme ulio na viwango vikubwa vya volteji na kuanzia kuunganisha nyumba yake na umeme kinyume na sheria.
Katika kibarua hicho chake, marehemu alijihami na pea ya koleo (pliers) tu.
Aligongwa na umeme huo vile vile na kuangushwa chini.
Wasamaria wema walioona kilichotokea, walimkimbiza katika hospitali moja iliyo karibu wakijaribu kuokoa maisha yake lakini alitangazwa mfu alipowasilishwa hospitalini.