Habari

Mudavadi asihi wakazi wa Malava wasimtie aibu, wachague mgombeaji wa UDA

Na MOSES NYAMORI, SHABAN MAKOKHA July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UCHAGUZI mdogo unaonukia eneobunge la Malava unatarajiwa kuwa mtihani mgumu kwa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ikizingatiwa chama chake kilichovunjwa cha ANC kilikuwa kikishikilia kiti hicho.

Bw Mudavadi ametangaza kuwa ataongoza kampeni za UDA ambayo kinara wake ni Rais William Ruto.

ANC ilivunjwa na kuungana na UDA mapema mwaka huu.

Marehemu Malulu Injendi ambaye alikuwa mbunge wa eneo hilo, alichaguliwa kupitia ANC mnamo 2022.

Bw Injendi aliaga dunia mnamo Februari 17, 2025 akiwa kati ya wabunge saba walioshinda viti kupitia ANC mnamo 2022.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2013 kupitia chama kisichokuwa na umaarufu cha MDP kisha akatetea kiti hicho 2017 na 2022 kupitia ANC.

Matokeo ya uchaguzi huo ni mtihani kwa Bw Mudavadi ambaye amekuwa akichukuliwa kuwa kigogo wa siasa za Magharibi japo mara si moja amelemewa kudhihirisha ubabe wake.

Amekuwa akilemewa katika kila uchaguzi na Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye amekuwa akipigwa kura kwa wingi na wakazi wa Magharibi.

Hata hivyo, tangu 2013, Bw Mudavadi amekuwa akitamba kwenye siasa za eneobunge la Malava ambako amekuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya Wakabras.

Alimshinda Bw Odinga katika kura ya 2013 eneobunge hilo kisha Bw Injendi, mwaniaji wake akawabwaga wawaniaji wa ODM 2017 na UDA na ODM mnamo 2022.

Mnamo Alhamisi, Kinara wa Mawaziri alikutana na zaidi ya wenyekiti 100 wa koo mbalimbali na wazee kutoka koo 29 za Kabras ambalo ni kabila kubwa ndani ya Malava.

Aliwaambia wazee hao nia yake ya kuhakikisha UDA imeshinda kiti hicho ili kuendeleza uwajibikaji ulioanzishwa na marehemu mbunge wao.

“Mimi ndiyo mlezi wenyu hadi mchague mbunge mpya. Lazima tushirikiane na tusonge mbele kwa kuweka msingi imara ulioachwa na marehemu ndugu yangu Injendi. Lazima tuhakikishe miradi ya maendeleo inaendelezwa na kukamilishwa,” akasema Bw Mudavadi.

Kiongozi huyo aliwataka wazee hao kuwaongoza wakazi kuamua mwaniaji bora ambaye atatea maslahi yao na anayeunga mkono utawala wa sasa.

“Nimetembea na nyinyi nyakati ngumu na wakati wa furaha. Sasa nawaomba, tuchague mbunge wa UDA ambaye atafanyakazi nami na Rais, mtu ambaye ataendeleza ajenda ya Malava hadi kiwango cha kitaifa,” akasema Bw Mudavadi.

Tayari kampeni zimeanza kunoga Malava hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini kutangaza siku ya kura.

DCP inayoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, DAP K ya Eugene Wamalwa ni kati ya vyama ambavyo vimeanza kampeni eneobunge hilo.

ODM na Ford Kenya bado hazijaweka wazi iwapo, zote zitakuwa na mwaniaji katika uchaguzi huo mdogo ambao tayari umewavutia wawaniaji zaidi ya 30.