Habari

Mudavadi atetea Rais Suluhu kuhusu wanaharakati ‘kuingilia’ masuala ya Tanzania

Na WINNIE ONYANDO May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKUU wa Mawaziri, Musalia Mudavadi ametetea matamshi ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu kuhusu wanaharakati wa Kenya kuingilia masuala ya utawala nchini mwake.

Haya yanajiri huku mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi akiendelea kuzuiliwa Tanzania.

Akizungumza Jumanne usiku (Mei 20, 2025) katika Citizen TV, Bw Mudavadi alikiri kwamba maoni ya Rais Suluhu kuhusu wanaharakati “kuingilia” masuala ya Tanzania yanaonyesha ukweli fulani.

“Sitapinga hilo kwa sababu nadhani kuna ukweli fulani. Hebu tukabiliane na mambo machache. Kiwango cha adabu, matusi, tunachoona nchini Kenya, ingawa tuna uhuru wa kujieleza, wakati mwingine kinazidi kupita kiasi. Ni ukweli anavyosema kuwa wakati mwingine matamshi yetu huku Kenya hupita kiasi,” alieleza Bw Mudavadi.

Aliongeza kuwa Wakenya wakati fulani wanakosa uadilifu katika matamshi yao.

“Mimi pia ni Mkenya, na ukweli wa mambo ni kwamba mtazamo wetu na matamshi yetu, kwa sababu tuna uhuru wa kujieleza, yamekosa uadilifu,” alisema.

Alipoulizwa ni kwa nini alimuunga mkono Bi Samia licha ya kutotaja uhalifu wowote uliofanywa na wanaharakati hao, Bw Mudavadi alisema anahitaji maelezo zaidi kuhusu operesheni hiyo.

“Yeye (Samia) amesema hana furaha, kwa sababu wanaangalia tunachofanya hapa, lakini nitahitaji muda kidogo kupata ushahidi zaidi kuhusu operesheni hiyo. Sizungumzii watu husika, lakini anazungumza kwa mtazamo wa jumla, na kama ni mtazamo wa jumla, basi nadhani ana hoja,” alisema.

Kando na hayo, Bw Mudavadi pia alifafanua kuwa ingawa uhuru wa kujieleza ni muhimu, kipaumbele cha rais kilikuwa kutetea uhuru wa nchi yake (Tanzania).