Habari

Mudavadi atofautiana na Ruto kuhusu kuwapiga waandamanaji risasi

Na CECIL ODONGO July 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KINARA wa mawaziri Musalia Mudavadi ametofautiana na Rais William Ruto huku akivitaka vyombo vya usalama visiwaumize Wakenya wakati wa maandamano.

Kwa mujibu wa Bw Mudavadi, Wakenya wanatekeleza tu majukumu yao ya kikatiba. Hata hivyo, amewataka Wakenya wanaoandamana nao pia waheshimu haki za wengine kwa kuwa huo ndio msingi wa demokrasia.

“Tufikirie na tutathmini haki zetu ninapowaomba maafisa wetu wa usalama wasiwajeruhi raia wanaoandamana. Wale wanaoandamana nao pia waheshimu haki za wengine,” akasema Bw Mudavadi katika video ambayo imesambaa mitandaoni.

Kauli yake inakuja baada ya Rais William Ruto wiki jana kuwataka polisi wawalenge kwa risasi wanaoandamana miguuni ili waende hospitalini na pia kuwajibikia mashtaka kortini.

Rais Ruto alisema japo hajaamrisha wauawe, polisi lazima wakabili wahalifu kwa mujibu wa sheria.