Mudavadi azomewa Embu kwa kudai uongozi kupitia uchaguzi ni bora kuliko wa kijeshi
KINARA wa Mawaziri Musalia Mudavadi amewahakikishia Wakenya kuwa uchaguzi mkuu ujao hautakuwa na hila zozote akieleza matumaini yake Rais William Ruto atachaguliwa kuhudumu kipindi cha pili.
Bw Mudavadi alisema kuwa utawala wa sasa unatekeleza jukumu lake vyema na utahakikisha kura hiyo inaandaliwa kwa njia ya huru na haki.
“Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) sasa ina makamishina wote na uchaguzi utakuwa huru na haki,” akasema Bw Mudavadi.
Alikuwa akiongea katika Shule ya Sekondari ya Kutus, eneobunge la Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.
“Tunataka kila mtu afahamu tuna serikali ambayo inajukumika, na Wakenya wafahamu kuwa njia pekee ya kubadilisha serikali ni kupitia debeni. Hii ndiyo maana kunafaa kuwa na uchaguzi kila baada ya miaka mitano na tangu uhuru hatujawahi kukosa kuandaa uchaguzi,” akaongeza.
“Wale ambao wanafikiria kuna njia nyingine wanakosea, kwa sababu lazima iwe ni kupitia debe. Lazima tuongee na ukweli huo ndio utahakikisha kuwa tuko huru,” akasema.
Kinara huyo wa mawaziri aliwaambia wale wanaomezea mate nyadhifa mbalimbali wajiandae kuwania kwa sababu Wakenya nao wanaonekana kuwa na ari ya kuwachagua viongozi wapya.
Hata hivyo, kinara huyo wa mawaziri alijipata pabaya na kuzomewa alipodai serikali iliyochaguliwa ni bora kuliko ile inayoongozwa na jeshi.
“Msihadaike au kudanganywa na mtu, Kenya huandaa uchaguzi kila baada ya miaka mitano kuwa na serikali dhabiti kwa sababu ndiyo bora kuliko utawala wa jeshi,” akasema huku wananchi wakimzomea na kusema ‘uongo, uongo’
Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah ambaye alikwepo katika mkutano aliwataka Wakenya wawachague viongozi kwa kuzingatia rekodi yao ya maendeleo.
“Wanaoomba kura zenu kwenye uchaguzi mkuu ujao, wanastahili kuonyesha kile ambacho wamefanya kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” akasema.
Mbunge huyo wa Kikuyu alisisitiza kuwa utawala wa Rais Ruto unamakinikia kutimiza ahadi zote za maendeleo kabla ya 2027.
“Kwa sasa tunamakinikia miradi ya maendeleo na uchaguzi ukija, tutawaonyesha kile ambacho tumewafanyia,” akasema.
Kati ya miradi wakazi wa Mbeere waliahidiwa ni serikali kutumia Sh170 milioni kuunganishia nyumba umeme.
Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano William Kabogo naye alisema atahakikisha kuwa kila wadi kitaifa ina intaneti.
Mbunge wa eneo hilo Nebart Muriuki alisema serikali inawekeza zaidi kwenye ngome zake za kisiasa na wakazi wana furaha.
“Mimi na watu wangu hapa tuko kwa hii serikali wala hatuondoki,” akasema Bw Muriuki.
Wakati wa hafla hiyo ya kuchangishia makundi ya akina mama, Bw Mudavadi alitoa Sh1 milioni.
Rais Ruto na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki nao walituma Sh3 milioni na Sh1.5 milioni mtawalia.