Mudavadi: Sh120 milioni zaidi zinahitajika kuokoa Wakenya Thailand, DRC
WIZARA ya Masuala ya Kigeni sasa inataka itengewe Sh120 milioni zaidi kufadhili shughuli ya kuwaokoa na kuwarejesha nyumbani Wakenya waliokwama katika nchi zinazokumbwa na misukosuko za Thailand, Lebanon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni jana ilisema Hazina Kuu haijatoa fedha zaidi za kufadhili shughuli hizo kulingana na maombi yaliyowasilishwa kwenye Bajeti ya Ziada.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Nelson Koech, jana alisema kuwa Idara ya kushughulikia Maslahi ya Wakenya walio ughaibuni inahitaji pesa hizo ili kuwaokoa Wakenya walio taabani katika nchi hizo zinazokumbwa na vita.
“Fedha hizo za ziada ni za kugharimia kuokolewa kwa Wakenya wanaokumbwa na hatari katika mataifa ya
Lebanon, Thailand na DRC,” akasema.
Mbunge huyo wa Belgut aliambia Kamati Shirikishi chini ya mwenyekiti Naibu Spika Gladys Boss Shollei kujumuisha mgao wa fedha hizo katika Bajeti ya Ziada ya II ya mwaka wa kifedha wa 2024/25.
Kamati hiyo inachambua mgao wa ziada wa Sh199 bilioni ambazo Hazina ya Kitaifa inaomba ziidhinishwe na Bunge kabla ya kutumika.
Hazina ya Kitaifa ilikuwa imeitengea Idara ya Masuala ya Wakenya walioko Ughaibuni Sh637.83 milioni lakini ikapunguza katika bajeti ya ziada ya pili hadi Sh633.7 milioni.
“Hii inaashiria kuwa Sh4.13 milioni zimepunguzwa kutoka mgao wa mishahara ya wafanyakazi,” Bw Koech akasema.