Habari

Munya azindua bodi mpya ya KFA

October 1st, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WAZIRI wa Biashara na Vyama vya Ushirika, Peter Munya siku ya Jumatatu alizindua bodi mpya ya shirika la Kenya Farmers Association (KFA).

Kulingana na waziri Munya, hatua hiyo inafuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta mnamo mwezi Julai kuwa wizara hiyo inafaa kuchukua hatua katika kufufua shirika hilo.

Bodi hiyo inachukua nafasi ya ile ya zamani ambayo imelaumiwa kwa kusababisha shughuli za shirika hilo kukwama.

Waziri Peter Munya (wa tatu kutoka kulia) alipokutana na wanakamati wa bodi mpya ya KFA siku ya Jumatatu, Septemba 30, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Magdalene Wanja

Kulingana na waziri Munya, bodi hiyo mpya itahudumu kwa miezi sita peke yake na baadaye, wakulima watachagua bodi mpya watakayopendelea iwaongoze.

“Bodi hii ni ya muda tu na katika kipindi cha miezi sita ofisini, inatarajiwa kufufua shughuli zilizokwama chini ya bodi ya zamani na kuwapa wakulima matumaini,” alisema Bw Munya.

Deni kubwa

Bw Munya aliilaumu bodi ya hapo zamani kwa kusababisha deni kubwa kwa shirika hilo.

“Shirika la KFA lina madeni makubwa kutoka kwa benki na wafanyakazi wake wa zamani,” aliongeza Bw Munya.

Aliongeza kuwa, kinyume na sheria, bodi hiyo haikufanya mikutano yoyote ya kila mwaka – AGM – na hivyo kuifanya kuwa ofisini kinyume cha sheria.

Shirika hilo lilianzishwa mnamo mwaka 1923 na liliwasaidia wakulima kuuza mapato kama vile maziwa, pareto, kahawa, mahindi na majanichai.