Murkomen amkingia Ruto dhidi ya shutuma za kutangaza ‘kiholela’ kifo cha afisa Kabiru Haiti
WAZIRI wa Usalama Kipchumba Murkomen amemkingia Rais William Ruto baada ya shutuma kuzuka kuhusiana na jinsi alitangaza kifo cha afisa wa polisi Benedict Kabiru.
Rais Ruto alitoa ufichuzi huo ulioshtua familia ya Kabiru na Wakenya kwa jumla, alipokuwa akihutubia kongamano la Umoja wa Mataifa jijini New York, Amerika.
Hata hivyo, Bw Murkomen anasema kufikia wakati Rais alikuwa anatoa tangazo hilo, ujumbe wa maafisa wa polisi ulikuwa njiani kwenda nyumbani kwa kina Kabiru na haukuwa umefika.
“Kikosi tayari kilikuwa njiani kwenda kueleza familia ya Kabiru kufikia wakati Rais alikuwa anazungumza. Familia hatimaye ilielezwa kuhusu kifo cha afisa huyo na tutaendelea kushirikiana kwa karibu na familia kuhusu suala hili,” akasema.
Waziri huyo hata hivyo hakuzungumzia kuhusu uliko mwili huo akisema kwamba habari zitatolewa katika muda ufaao.
Kabiru alikuwa katika ujumbe wa kwanza uliopelekwa kudumisha amani katika taifa hilo la visiwa vya Caribbean ambako magenge hatari yanatawala.
Habari za kutoweka kwa Kabiru zilifichuliwa kwa mara ya kwanza na Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja mnamo Machi 25 mwaka huu. Tangu wakati huo, imekuwa miezi sita ya kimya cha serikali.
Jumatano, familia ya Kabiru ilifika mahakamani kutaka serikali ilazimishwe kutoa taarifa kuhusu hali ya mwana wao.