Murkomen: Bundiki tano na risasi 14 zimetwaliwa Trans Mara
BUNDUKI haramu tano na risasi 14 zimesalimishwa kwa polisi Angata Barrikoi, Transmara katika Kaunti ya Narok kufuatia mapigano makali ya kikabila ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu wanne na mamia ya wakazi kuhama makwao.
Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen idadi hiyo ni ya chini kwa sababu bado kuna zaidi ya bunduki 100 haramu bado ziko mikononi mwa raia.
“Hilo ni tone katika bahari ikizingatiwa kuwa eneo hili linakadiriwa kuwa na takriban bunduki 100 haramu. Vyombo vyetu vya usalama vimepewa maagizo thabiti ya kusaka silaha zote zilizosalia,” akasema Bw Murkomen.
Waziri huyo alizuru eneo hilo jana akiandamana na maafisa wakuu wa usalama na kuongeza kuwa bunduki zote haramu mikononi mwa raia katika maeneobunge ya Kilgoris, Kuria Magharibi, Kuria Mashariki na Emurua Dikirr lazima zirudishwe bila kuchelewa.
Aliongeza kuwa operesheni za usalama katika eneo hilo lililoathiriwa zimeimarishwa.
Bw Murkomen pia alidokeza kwamba walinzi wote wa wanyamapori na mbugaNarok watalazimika kufanyiwa ukaguzi upya, akiongeza kuwa imebainika kuwa baadhi yao walikuwa wakitumia bunduki zao vibaya.
” Nitatoa agizo la sera kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kuhakikisha kwamba walinzi hao wote nchini wanakaguliwa upya, wanafanya kazi chini ya muundo ulio wazi wa kuripoti, na kubaki kuwajibika kikamilifu kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi,” akaongeza.
Takriban watu sita wamekamatwa kuhusiana na mapigano hayo yanayoendelea. Miongoni mwa sita hao ni Mwakilishi wa Wadi (MCA) na afisa wa polisi wa cheo cha konstebo.
Walifikishwa katika mahakama ya Nakuru siku ya Jumatatu ambapo walishtakiwa kwa makosa mbalimbali miongoni mwao ya kuchochea ghasia, uchomaji moto, kuendeleza shughuli zinazoleta vita miongoni mwa tuhuma zingine.