Habari

Muthama kuitwa kutoa ushahidi katika kesi ya ughushi wa cheti cha kuzaliwa

August 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Seneta Kaunti ya Machakos Johnstone Muthama ameorodheshwa kuwa shahidi katika kesi ya ughushi wa cheti cha kuzaliwa mtoto miaka 17 iliyopita dhidi ya Nina Maria Wanjiku.

Wanjiku aliyetiwa nguvuni na polisi Mombasa Agosti 1, 2025 alishtakiwa Jumatatu (Agosti 4, 2025) mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi.

Wanjiku alikana mashtaka mawili aliyoshtakiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga.

Mahakama ilielezwa na wakili wa Serikali Sonia Njoki kwamba Wanjiku alighushi cheti hicho cha kuzaliwa kwa mtoto (jina limebanwa ili kulinda haki zake) mnamo Janauri 28, 1998.

Mshtakiwa alikana alighushi cheti nambari 300868 akidai ni halali kutoka kwa msajili wa watoto.

Mahakama ilifahamishwa mnamo Mei 21, 1998, Wanjiku alimkabidhi afisa wa Uhamiaji cheti hicho cha kughushi alipoenda kumchukulia mtoto huyo pasipoti.

Nina Maria Wanjiku aliyeshtakiwa mahakama ya Milimani Agosti 4 kwa kughushi cheti cha kuzaliwa cha mtoto. Picha|Richard Munguti

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “atatii masharti atakayopewa na kwamba atafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi.”

Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Katika uamuzi wake, Bw Ekhubi alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa afikishwapo korti.

Alisema mshtakiwa anaweza kunyimwa haki hiyo endapo korti itaelezwa atatoroka ama kuvuruga mashahidi.

“Hii mahakama imetilia maanani upande wa mashtaka haupingi ukiachiliwa kwa dhamana. Umeachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000,” hakimu alimweleza mshtakiwa.

Mahakama ilitenga kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kusikizwa.

Hakimu pia aliamuru mshtakiwa apewe nakala za ushahidi aandae tetezi zake.

Wanjiku alieleza mahakama kwamba alitiwa nguvuni Mombasa na kusafirishwa hadi kituo cha polisi cha Gigiri alikotolewa kushtakiwa kortini.

Mbali na Muthama mashahidi watatoka idara ya usajili na idara ya uhamaji.