Muthaura ataka serikali ya 'nusu mkate'
Na BENSON MATHEKA
ALIYEKUWA Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, anapendekeza katiba irekebishwe ili mgombea urais anayeibuka wa pili kwenye uchaguzi mkuu ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.
Bw Muthaura alisema katiba inafaa kubadilishwa ili kuruhusu mgombea urais anayepata kura nyingi kwenye uchaguzi wa urais kuunda serikali ya muungano na anayeibuka wa pili.
Akitoa mapendekezo yake Alhamisi mbele ya kamati ya maridhiano (BBI), inayokusanya maoni kutoka kwa umma, Bw Muthaura alisema kwamba mshindi wa uchaguzi wa urais, anapaswa kuwa rais na kiongozi wa taifa, naye anayechukua nafasi ya pili anafaa kuteuliwa waziri mkuu.
Kulingana na Bw Muthaura ambaye alihudumu katika serikali ya muungano chini ya Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga kati ya 2007 na 2013, pendekezo lake likikubaliwa, litakomesha ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
Alitoa mfano wa uchaguzi mkuu uliopita ambapo Bw Odinga aliyeibuka wa pili alijiapisha kuwa rais wa wananchi.
“Mara nyingi, mtu anayeibuka wa pili huwa na ufuasi wa takriban asilimia 40 ya nchi. Hii ni sehemu kubwa ya nchi ambayo haifai kupuuzwa,” alisema.
Hata hivyo, aliambia kamati hiyo kwamba wadhifa wa Naibu Rais haufai kufutiliwa mbali akisema ni muhimu kwa sababu za urithi kiti cha rais kikibaki wazi.
Katika pendekezo lake, Bw Muthaura alisema baraza la mawaziri linafaa kuundwa na Rais akishirikiana na Waziri Mkuu lakini akaongeza ni kiongozi wa taifa pekee anayepaswa kuwa na nguvu za kuachisha kazi mawaziri.
Bw Muthaura alisema pendekezo lake litazuia nchi kugawanyika na kuzuia ghasia za kikabila na kisiasa ambazo hutokea nchini kila baada ya uchaguzi.
Alitoa mfano wa serikali ya muungano aliyohudumu ambayo ilibuniwa baada ya ghasia za 2007/2008 na muafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga uliotuliza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa 2017. “Handisheki hii inapaswa kuwa sehemu ya katiba kupitia marekebisho kuhakikisha kuna ugavi wa mamlaka chini ya serikali ya muungano wa kitaifa ambayo itaimarisha uwiano,” alisema.
Kulingana na Bw Muthaura, waziri mkuu anafaa kusimamia baraza la mawaziri kwa kutumia mamlaka anayopatiwa na rais.
Aidha, alipendekeza Rais na Waziri Mkuu wawe wakigawana viti vya uongozi bungeni.
Mawaziri
Alijiunga na wanaotaka mawaziri kuteuliwa kutoka kwa wabunge akisema kwa wakati huu kuna mwanya kati ya bunge na serikali kwa sababu mawaziri si wabunge.
Kwa kutoa mapendekezo hayo, Bw Muthaura alijiunga na viongozi wengine wanaounga marekebisho ya katiba.
Viongozi wa kisiasa, wakiwemo wabunge, magavana maseneta na vyama vya wafanyakazi wamekuwa wakiambia kamati hiyo kwamba kuna haja ya kubadilisha muundo wa serikali ili kupunguza mamlaka ya rais, kuimarisha ushirikishi na kujenga uwiano nchini.
Miongoni mwa wanaopigia debe marekebisho ya katiba ni kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye anapendekeza wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wawili.
Hata hivyo, Naibu Rais anapinga kubuniwa kwa wadhifa huo akisema ni kuongezea Wakenya gharama ya kuendesha serikali.