Habari

Muturi aendelea kupapasa mamba, je, hahofii kutafunwa?

Na CHARLES WASONGA March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

WAZIRI wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ameendelea kuikosoa serikali na kukwepa kuhudhuria mikutano ya baraza la mawaziri huku akishikilia kuwa hatajiuzulu ndani ya utawala wa Kenya Kwanza.

Nacho chama chake, Democratic Party-DP, kimetoa ilani ya kujiondoa katika muungano tawala wa Kenya Kwanza, hali inayotilia shaka imani yake kwa serikali.

Hata hivyo, wandani wa Rais William Ruto, wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, wanashikilia kuwa siku zake katika baraza la mawaziri ni za kuhesabika kwani atapigwa kalamu hivi karibuni.

Kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen Jumatano usiku, Bw Muturi alifichua kuwa hatahudhuria vikao vya baraza la mawaziri hadi pale ajenda ya utekaji nyara na mauaji ya kiholela, yanayotekelezwa na maafisa wa usalama, itakaporatibiwa kujadiliwa.

Waziri huyo alieleza kuwa japo ni lazima kwa mawaziri wote kuhudhuria vikao hivyo, isipokuwa kwa wale waliopata kibali cha kukosa kufika, kutoka kwa rais, ameomba kutohudhuria mikutano hiyo.

“Niliwasilisha barua kwa Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa vikao vya baraza la mawaziri kwamba nisingehudhuria. Ikiwa suala nyeti la Wakenya kutekwa nyara na wengine kupatikana wameuawa halitaorodheshwa kwenye ajenda ya mikutano hiyo, basi sote kama mawaziri ni wahusika katika uovu huo,” Bw Muturi akaeleza.

Alisisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuwasilishwa rasmi katika baraza la mawaziri ili serikali itangaze msimamo wake na kutoa mwelekeo kuhusu namna ya kukabiliana nalo. Bw Muturi amekosa kuhudhuria mikutano mitatu ya baraza la mawaziri; mnamo Januari 21 katika Ikulu ndogo ya Kakamega, Februari 11 na Machi 11, 2025 katika Ikulu ya Nairobi.

Mnamo Juni mwaka jana, mwanawe Muturi, Lesly, alitekwa nyara katika eneo la Kilimani, Nairobi akiwa na Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje. Hata hivyo, aliachiliwa baada ya siku chache.

Mnamo Januari 4 mwaka huu, Waziri Muturi alijitokeza waziwazi na kukizungumzia kisa hicho kadamnasi akidai ilimlazimu kumpigia simu Rais Ruto ndipo mwanawe akaachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa siku kadhaa na maafisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS).

Kwenye kikao na wahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, waziri huyo aliikashifu vikali serikali kwa kudai haikuwajua watu waliowateka nyara vijana saba Desemba 2024.

“Serikali haiwezi kudai kwamba haijui kile kinachoendelea huku familia za vijana saba waliotekwa nyara zikiendelea kuhangaika. Binafsi niliwahi kupitia hali kama hii mwanangu alipotekwa nyara miezi sita iliyopita,” Bw Muturi akaeleza.

Jumatano, waziri huyo pia alielezea jinsi ushauri wake kuhusu miswada ya serikali na masuala mbalimbali yalivyopuuzwa alipokuwa akihudumu kama Mwanasheria Mkuu.

“Kupuuzwa kwa ushauri wangu ndiko kulichangia kutupiliwa mbali kwa miswada mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC). Isitoshe, sikuhusishwa katika utayarishaji wa miswada hiyo, nilishtukia imewasilishwa bungeni bila kupitishwa afisini mwangu kama mwanasheria mkuu,” akaeleza.

Juzi, shinikizo za kumtaka Bw Muturi ajiuzulu zilishika kasi pale waziri huyo alipoikosoa serikali kwa kuanzisha miradi mipya ilhali miradi ya zamani imekwama.

Akitoa kauli za wizara yake kuhusu Taarifa ya Kisera kuhusu Bajeti ya 2025 mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Leba, Bw Muturi alieleza kuwa miradi kadhaa ya maendeleo imetelekezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Alidadisi mantiki ya kuanzishwa kwa miradi mipya badala ya kukamilisha ile iliyoanzishwa karibu miaka 10 iliyopita.

“Sijui ikiwa kuna kosoro fulani mawazoni mwetu kama serikali. Nimezuru maeneo kadhaa nchini na kushuhudia miradi iliyokwama kwa zaidi ya miaka 30. Kwa mfano, nilitembelea mji wa Wote, Makueni na kuona nyumba kadhaa zilizoanza kujengwa miaka 20 iliyopita lakini zimekwama. Sasa mbona tunatumia pesa za umma kwa ujenzi wa nyumba nyingine za gharama nafuu badala ya kukamilisha hizi?”akauliza Bw Muturi mbele ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Runyenjes Eric Karemba.

Kauli hiyo ilimkasirisha Mbunge wa Belgut Nelson Koech aliyemshutumu Bw Muturi kwa kukosoa sera na mipango ya serikali ya Rais Ruto.

“Huyo Muturi atafutwa kazi siku chache zijazo. Hafai kukosoa mipango ya serikali anayoihudumia. Ikiwa hana imani na serikali hii aondoke au afurushwe ndani ya wiki chache zijazo,” akafoka Bw Koech, ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Ruto.