Mutyambai aamuru kukamatwa kwa afisa aliyempiga risasi mwanamume eneo la Lessos
Na CHARLES WASONGA
INSPEKTA JENERALI wa Polisi Hillary Mutyambai Alhamisi jioni aliamuru kukamatwa na kusimamishwa kazi kwa afisa wa polisi ambaye inadaiwa alimpiga risasi na kumuua mwanamume mmoja eneo la Lessos, Kaunti ya Nandi.
Kisa hicho kilitokea baada ya mwendesha bodaboda aliyekuwa akisafirisha abiria wawili alipokamatwa kwa kutovalia barakoa.
Kulingana na Bw Mutyambai, wanabodaboda wengine walimshambulia polisi aliyejaribu kumkamata mwenzao ambaye hakuwa amevalia barakoa na kujaribu kumpokonya afisa huyo bunduki yake, alipokuwa akimpeleka mshukiwa katika kituo cha polisi cha Lessos.
Katika fujo zilizotokea, Lazarus Kirop, 40, alipigwa risasi na akafariki.
Baadaye wananchi wenye ghadhabu walijaribu kuteketeza kituo hicho cha polisi.
Vilevile, raia walijaribu kuharibu nyumba ya afisa wa polisi mwenye cheo cha juu na kuchangia vifo vya watu wengine wawili.
“Idara ya Polisi nchini Kenya inakariri kujitolea kwa kuwahudumia watu wote kwa usawa chini ya kauli mbiu ya “Utumishi kwa Wote”. Na hakuna afisa ataruhusiwa kuchukua sheria mikononi mwake,” ikasema taarifa kutoka kwa msemaji wa polisi Charles Owino.
Ikaeleza: “Tumeagiza Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (Ipoa) kuchukua hatua jinsi inavyofafanuliwa kisheria. Tutawaadhibu maafisa wote ambao watapatikana na kosa na kudhihirisha mienendo inayokiuka sheria.”
Bw Mutyambai alisema kuwa sheria ya polisi bado inashikilia “maafisa wote wa polisi wanaokiuka sheria hawatasamehewa, hata kama walifanya hivyo wakiwa kazini.”
“Maafisa wa polisi wanafaa kutekeleza wajibu wao kitaaluma huku wakidumisha ushirikiano na umma katika jitihada zao za kuhakikisha kuna usalama katika jamii,” akasema.