Habari

'Mvua iliyopitiliza kiwango kuendelea kunyesha hadi Desemba 4'

November 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetangaza mvua iliyopitiliza kiwango itaendelea kushuhudiwa maeneo ya South Rift, Central Rift na Nyanza kuanzia jana Ijumaa, Novemba 29 hadi Desemba 4, 2019.

Iliongeza kuwa kuna uwezekano wa mvua hiyo kuenea hadi maeneo ya Kati mwa Kenya, Nairobi na maeneo ya Kusini Mashariki.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na mkurugenzi mmojawapo wa idara hiyo David Gikungu, idara hiyo iliwataka Wakenya kuchukua tahadhari ili kuzuia kutokea kwa maafa na uharibifu wa mali.

“Mvua ya kiwango cha zaidi ya milimita 30 ndani ya saa 24 inatarajiwa kushuhudiwa kuanzia Ijumaa (jana) Novemba 29, 2019 katika maeneo ya South Rift, Central Rift na Nyanza,” ikasema taarifa hiyo.

Kaunti ambazo zinatarajiwa kushuhudia mvua kiwango kikubwa ni pamoja na Narok, Kajiado, Bomet, Kericho, Nakuru, Migori, Nyamira, Kisii, Homa Bay, na Siaya.

Zingine ambazo pia zinatarajiwa kushuhudia kiasi hicho ni Nairobi, Nyeri, Murang’a, Kiambu, Nyandarua, Kirinyaga, Machakos, na Makueni.

“Watu wanaoishi katika maeneo ambayo huathirika na maporomoko ya ardhi kama vile Pokot Magharibi na Murang’a, milima ya Aberdare, Mlima Kenya na maeneo mengine wanatakiwa wawe makini,” idara hiyo ikaonya.

Wale wanaoishi katika maeneo yenye uwezekano wa kuathirika na mafuriko au maporomoko ya ardhi wameshauriwa kuhamia maeneo salama.

Mnamo Novemba 22 mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi katika kaunti ya Pokot Magharibi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30 huku wengine ikiwa bado haijulikani waliko.

Vijiji vilivyoathiriki ni pamoja na Nyarkulian, Parua, Seit na Muino katika eneobunge la Pokot Kusini.

Watu wanaoishi katika maeneo haya wameshauriwa kuhamia maeneo salama.

Serikali nchini Kenya imesema maafa kutokana na mafuriko na kadhia nyinginezo zinazosababishwa na mvua katika kipindi cha miezi michache tayari imefika zaidi ya watu 100.