Habari

Mvutano wa udhibiti wa Sh60 bilioni za mishahara ya polisi wafika Mahakama Kuu

Na RICHARD MUNGUTI August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imeombwa itatue mzozo kuhusu udhibiti wa mishahara ya Idara ya Polisi ya Sh60 bilioni kati ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja na tume ya huduma ya kitaifa ya asasi hiyo ya usalama (NPSC).

Katika kesi iliyowasilishwa na vuguvugu la Sheria Mtaani lake wakili Shadrack Wambui, Jaji Lawrence Mugambi ametakiwa aamue kati ya  IG na NPSC aliye na usemi kuhusu mabilioni hayo ya mishahara.

Bw Wambui anaomba mahakama kuu ishurutishe IG ajitenge na masuala ya mishahara na atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa kifungu nambari 245 cha Katiba.

Korti imeelezwa majukumu ya IG ni ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.

Bw Wambui pia anaomba mahakama kuu itangaze kwamba NPSC ndio inapasa kushughulikia masuala ya mishahara na kuadhibu maafisa watovu wa nidhamu kwa mujibu wa kifungu nambari 246 cha Katiba.

Katika kesi hiyo, mawakili Danstan Omari na Wambui wamemshtaki IG, huduma ya kitaifa ya polisi (NPS) na mwanasheria mkuu.

Wameomba mahakama kuu iwape idhini wawasilishe kesi hii chini ya sheria za likizo ya mahakama kuu ndipo masuala nyeti ya katiba katika mtafaruku huu wa udhibiti wa Sh60 bilioni yaamuliwe.

Wengine walioshtakiwa ni NPSC na Chama cha mwakili nchini (LSK).

Bw Omari ameeleza mahakama kwamba mzozo kati ya IG na NPSC kuhusu uthibiti wa mishahara ya polisi na ajira ya makurutu 10,000 wa polisi unasababisha mtafaruku wa kikatiba kuhusu “aliye na mamlaka juu ya maafisa hawa wa utumishi kwa wote.”

“Hivi punde kumezuka mtafaruku kati ya IG na NPSC kuhusu udhibiti wa mabilioni ya pesa za mishahara ya polisi. Utata na hali ya mshike mshike imekita mizizi katika asasi hii ya usalama,” Bw Omari amedokeza katika ushahidi aliowasilisha katika mahakama kuu.

Bw Omari ameeleza kwamba suala hilo linazua masuala mazito ya kikatiba yanayotakiwa kuamuliwa na mahakama kuu ndipo “ibainike mwenye mamlaka katika kikosi cha polisi ikiwa ni IG ama NPSC.”

“Je ikiwa IG ndiye anaongoza kikosi cha polisi na silaha za kikosi hicho ziko chini ya mamlaka yake, je itakuwa aje polisi wakisusia kazi kwa siku moja,” Bw Omari alihoji.

Mawakili hao wanaomba mahakama ifafanue vipengee nambari 245 na 246 vya katiba kuhusu utenda kazi wa kikosi cha polisi.

Kwa mujibu wa sheria NPSC ndiyo iko na mamlaka ya kuwaajiri na kuwapandisha vyeo maafisa wa polisi pamoja na kuadhibu polisi wapotovu.