Habari

Mwanafunzi mwenye dalili kama za virusi vya Corona alazwa KNH

January 28th, 2020 2 min read

NASIBO KABALE, MARY WANGARI na MASHIRIKA

MWANAFUNZI aliyetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) akiwa na dalili kama za virusi vya Corona ambavyo mara ya kwanza viliripotiwa Wuhan, mk0ni Hubei, China, na ambavyo kufikia sasa vimewaua watu zaidi ya 106 ametengewa chumba maalum chini ya uangalizi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Mgonjwa huyo husomea nchini China.

Wizara ya Afya inachunguza kisa hicho cha uwezekano wa virusi hivyo hatari.

Ingawa hajatajwa, ana umri wa ishirini au zaidi na alitua JKIA akiwa na dalili za virusi vya Corona na mara moja Wizara ya Afya ikawahi kumpeleka katika hospitali leo Jumanne saa tatu na nusu asubuhi.

Meneja wa mawasiliano wa KNH Bw Hezekiel Gikambi amesema  JKIA iliarifiwa na kuwekwa katika hali ya tahadhari kutoka kwa vitengo vinavyohudumu katika uwanja wa ndege.

“Ameletwa na ambulensi inayohudumu pale katika uwanja wa ndege na kufikia sasa anafanyiwa vipimo ama kuthibitisha au kubainisha vinginevyo kuhusu virusi vya Coronae,” amesema Bw Gikambi.

Kufikia sasa vimegundulika visa zaidi ya 4,500 vya virusi hivyo – idadi maradufu – tangu visa vya mwanzo mwanzo kuripotiwa Desemba 2019 kutoka Wuhan, China.

Baadhi tu ya dalili ni makamasi kutoka puani, kukohoa na uvimbe katika koo.

Pia waathirika wanaweza kuwa na maumivu ya kichwa pamoja na mwili kuchemka kwa siku kadhaa.

Haya yanajiri huku tayari Amerika na mataifa mengine yakifanya upesi kuwaondoa raia wao katika mji wa Wuhan uliowekewa mzingiro ambao ni kitovu cha mkurupuko wa virusi hivyo.

Virusi hivyo hatari ambavyo wataalamu wanaamini viliibuka kutoka soko kunakouzwa nyama na viungo vya wanyamapori katika jiji la Wuhan, vimefanya China ichukue juhudi kabambe za kudhibiti hali baada ya kusambaa kote nchini humo na katika mataifa mengine kadhaa.

Serikali ya taifa hilo imeifunga Wuhan na miji mingine katika mkoa wa kati wa Hubei na kuwafungia ndani zaidi ya watu 50 milioni, ikiwemo maelfu ya raia wa kigeni, katika juhudi za kudhibiti virusi hivyo, huku msimu wenye safari nyingi wa Mwaka Mpya China ukiwadia.

Huku walio Wuhan wakizidiwa na hofu, serikali za mataifa kadhaa zimeng’ang’ana kubuni njia za kuwaondoa salama raia wao nje ya mji huo wenye watu milioni 11.

Amerika, Ufaransa na Japan ni miongoni mwa mataifa ambayo yametangaza mipango ya usafirishaji kwa ndege lakini karibu wiki moja baada ya hatua ya kufunga mji huo, shughuli hiyo bado haijaanza ama kurejelewa.

Ndege iliyoidhinishwa ya Amerika ilipangiwa kuondoka Wuhan leo Jumanne ikiwa na wafanyakazi wa ubalozi na raia wa Amerika, lakini Idara ya Usalama wa Nchi ikasema shughuli hiyo ilikuwa imeahirishwa hadi Jumatano bila kutoa sababu.

Ufaransa pia imesema inanuia kuwasafirisha kwa ndege raia wake nje ya mji huo katikati mwa juma hili huku Japan ikiwa na mipango kama hiyo.

Mataifa mengine kadha pia yanajitahidi kuwaondoa watu wao nchini humo huku Ujerumani ikisema inatafakari kufanya hivyo.

Mamlaka ya Singapore imesema inafanya kazi pamoja na China ili kuwarejesha nyumbani raia waliokwama Wuhan.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Usafiri Singapore, Janil Puthucheary alisema maafisa wanawasiliana na raia wa Singapore ambao kwa sasa wamo mjini humo na wanasaka mbinu za kuwarejesha ikiwemo mashirika ya ndege.

Virusi hivyo vinaweza kuambukizwa baina ya watu ingawa wanasayansi bado hawajabaini kasi ya maambukizi yake na njia halisi za usambazaji wake.