Mwanaharakati Mwangi aliteswa na serikali ya Tanzania, familia yasema
IMEBAINIKA kuwa mwanaharakati Boniface Mwangi alipitia mateso mikononi mwa serikali ya Tanzania na sasa anahitaji matibabu ya haraka.
Hii ni kulingana na familia ya mwanaharakati huyo aliyepatikana ametelekezwa katika eneo la Ukunda Kaunti ya, Kwale.
Baada ya kupatikana kwake, familia yake ilimkimbiza hospitalini kwa ukaguzi.
Hata hivyo, haijabainika ni aina gani ya mateso Bw Mwangi alipitia akiwa mikononi mwa serikali ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu.
Habari za kurejeshwa kwake nchini ziligonga vichwa vya habari Alhamisi (Mei 22, 2025) muda mchache baada ya serikali ya Kenya kuingilia kati kutaka Tanzania imwachilie huru.
Katibu wa Wizara ya Masuala ya Nje, Dkt Abraham Korir Sing’Oei, siku iyo hiyo alilalamikia kutoweka kwa Bw Mwangi na akaiomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtoa au kumwachilia.
“Wizara inabaini kuwa licha ya maombi kadhaa, maafisa wa serikali ya Kenya wamezuiwa kupata taarifa na pia kumfikia Bw Mwangi. Wizara pia ina wasiwasi kuhusu hali yake ya afya, ustawi wake kwa ujumla na ukosefu wa taarifa kuhusu kuzuiliwa kwake,” alisema Katibu huyo katika taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.
Jumatatu, mkewe mwanaharakati huyo aliomba serikali ya Tanzania kutoa habari kuhusu aliko mume wake.
Wanaharakati wa Kenya wameungana na serikali kulaani hatua ya serikali ya Tanzania kumkamata.
Hii ni baada ya Rais wa Tanzania Samia kusema kuwa hataruhusu watu kutoka mataifa mengine kuleta vurugu nchini mwake.
“Tumeanza kuona mwenendo ambapo baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani wanajaribu kuingilia mambo yetu. Kama wamekomeshwa kwao, basi wasije kuvuruga amani yetu hapa,” alisema Mama Suluhu.