Mwanamke adai mshukiwa wa mauaji ya Kamto hakumlipa kwa ‘huduma zake’
MWANAMKE mmoja amelilia Mahakama ya Shanzu kuwa mshukiwa mwenzake katika mauaji ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Kilifi Kenneth Kamto alikosa kumlipa kwa huduma zake baada ya polisi kukatiza “shughuli” yao walipokamatwa.
Bi Florence Mwanza aliishangaza mahakama kwa kusema kuwa Bw Julius Gitonga hakumlipa baada ya kukamatwa kuhusiana na tukio hilo la Desemba 12, 2018, ambalo liligonga vichwa vya habari.
Bi Mwanza alikiri kushiriki ngono kibiashara na wanaume na katika tukio hili walifumaniwa na polisi.
“Hakunilipa kwa huduma zangu wakati polisi walipotukamata,” alimwambia Hakimu Mkuu Mwadamizi Yussuf Shikanda.
Pia, alikiri kwamba alipatikana kwa nyumba ya Bw Gitonga, akisema mwanamume huyo ni mteja wake wa muda mrefu na kwamba alikuwa akilipa kodi yake.
“Nilikuwa naye alipokamatwa. Polisi walinitoa nje walipoingia nyumbani mwake. Sikujua kama kulikuwa na bunduki nyumbani. Sijawahi kuona bunduki nyumbani kwake,” alisema.
Bi Mwanza alisema kuwa wakati fulani Gitonga angekopa pesa kutoka kwake ili kulipa kodi ya nyumba kabla ya kumrudishia baadaye.
“Nisingeingia nyumbani mwake kama ningejua alikuwa na bunduki. Nisingelipa kodi yake,” alisema.
Mwanamke huyo alisema ana wateja wengi, lakini siku hiyo alikuwa na Bw Gitonga, ambaye alikuwa ametoka kijijini na kuomba huduma zake.
“Sijawahi kuwalipia kodi wateja wangu wengine; Nilimlipia Gitonga kodi ya Sh3500 kwa mwezi mara kadhaa. Alikuwa mteja wangu kwa muda mrefu,” alisema.
‘Sina uhusiano na bunduki; hapakuwa na ushahidi wowote dhidi yangu. Hakuna silaha iliyopatikana katika nyumba yangu huko Bombolulu,” mwanamke huyo alisema.
Bw Gitonga alijitetea kuwa yeye ni mfanyabiashara wa miraa na muguka na kuwa alikuwa Meru wakati wa kisa hicho.
Mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 56 alisema aliondoka Mombasa Desemba 7, 2018 na kurejea Januari 6, 2019.
Alikana kuwafahamu washtakiwa wenzake isipokuwa Bi Mwanza.
“Ninamfahamu, niliwahi kumtembelea na kumlipa kwa huduma zake,” aliambia mahakama alipoulizwa na Kiongozi wa Mashtaka Ngina Mutua uhusiano wake na washtakiwa mwenzake.
Aliporejea Mombasa kutoka Meru, alieleza kuwa alienda moja kwa moja kumuona Bi Mwanza na kumtaka aandamane naye hadi nyumbani kwake kuisafisha.
“Nilimwambia kuwa nyumba yangu ilikuwa chafu na sikuwa na uwezo wa kulipia chumba cha wageni. Alitaka nimlipe Sh1000, lakini baadaye tukakubaliana Sh200. Tulifika nyumbani kwangu saa tatu unusu asubuhi,” alisema.
Majira ya saa kumi jioni, Bw Gitonga alisema alisikia mlango wake ukigongwa, na alipoenda kufungua, alikutana na mtutu wa bunduki na kuamriwa arudi ndani.
“Walikuwa wamevaa kiraia. Niliamriwa kuketi na mara nikafungwa pingu kwa nyuma. Mwanza alibururwa nje ya nyumba. Nilifungwa macho na kupigwa teke la mgongoni na kunifanya niangukie kwa tumbo,” alisema.
Alisema baada ya hapo alitolewa nje na kuingizwa kwenye gari la polisi na kupelekwa kituo cha polisi cha Mjambere ambako alihojiwa na baadaye kufunguliwa mashtaka mahakamani.
Kamto alikuwa amewasili nyumbani kwake mwendo wa saa nane asubuhi wakati watu wenye silaha walipovamia boma lake mara tu alipopita lango lake kuu.
Kufuatia kisa hicho, Bw Gitonga, Bw Joseph Amwayi Mukabana, Bi Mwanza, Bw Joseph Shoi Chege, Bi Clementina Nerima, na Bw Muasya Kiteme, almaarufu Mwaa, walishtakiwa kwa makosa kadhaa ya wizi wa kimabavu na kupatikana na vitu vya wizi.
Kiteme alifungwa jela miaka 15 miaka mitatu iliyopita baada ya kukiri kushiriki katika wizi na ufyatuaji risasi iliyomuua Bw Kamto.
Hata hivyo, Bw Chege na Bi Clementina waliachiliwa, na kuwaacha Bw Gitonga, Bw Mukabana, na Bi Mwanza wakipigania uhuru wao mahakamani.