Mwanamke aliyeandikia dadake WhatsApp kwamba atajiua apatikana amekufa Mto Yala
MWANAMKE ambaye Machi 5 mazungumzo na dadake yalichapishwa kwenye Facebook kuwa angetamatisha maisha yake kwa kujirusha kwenye Mto Yala, Kaunti ya Siaya, hatimaye amefanya hivyo.
Jumapili, mwili wa Mercy Nyasaka ulipatikana ukielea katika mto huo na unatarajiwa kufanyiwa uchunguzi leo.
Kamanda wa Polisi wa Gem Charles Wafula alithibitisha kisa hicho akisema mwili wake uliondolewa na umetambuliwa na mjomba wake John Odongo.
“Iliripotiwa na naibu chifu wa lokesheni ya Gongo Frank Owino baada ya umma kuona mwili wake ukielea kwenye eneo la Gongo,” Wafula akaambia Taifa Leo.
Bi Nyasaka alionekana kuandamwa na matatizo mengi na kwenye ujumbe aliomwaandikia dadake siku chache baada ya Machi 5, alifichua mpango wa kutaka kutamatisha uhai wake kutokana na mzigo mkubwa wa maisha.
“Hii ndiyo njia bora ambayo nimeona naweza kutumia kumaliza uchungu na kejeli ambazo hazijaisha maishani mwangu,” akaandika kwenye ujumbe huo.
Mnamo Machi 12, Bi Nyasaka alitoweka kutoka nyumbani kwao Mbita, Kaunti ya Homa Bay saa nne mchana na jamaa zake wakamsaka kisha kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kondele.
Kwenye ujumbe katika WhatsApp, Nyasaka aliweka wazi jinsi madeni yalivyokuwa yakimwaandama, matatizo ya ndoa na kuamua kujitoa uhai.
“Pole kwa kuwasikitisha lakini kufikia wakati mtapata ujumbe huu, nitakuwa nimeenda. Mtafute mwili wangu kwenye daraja la Sinaga, katika Mto Yala,” akasema.
Aidha, alimtaka dadaye amweleze mumewe amalize deni la gari la Sh50,000 ili gari lisitwaliwe. Bi Nyasaka pia alibainisha nambari ya mwanamke mwingine aliyemtambua kwa jina Beryl aliyekuwa akimdai deni la Sh300,000 na akaongeza kwamba mwanamke huyo alikuwa na hati miliki yake ya ardhi.
“Mwili wangu ukipatikana, mnizike nyumbani kwa mamangu au kwenye makaburi.
“Nitakuwa nikiwatazama. Wapende na uwaangalie watoto wangu kama wako,” Bi Nyasaka akamwomba dada yake.
Kwenye simulizi ya kina, alisema jinsi ambavyo ulimwengu ulimpasukia mnamo Machi 1, 2023 alipofiwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka 11.
Alisimulia jinsi ambavyo alishikwa na homa kali, mwili wake ukawa na joto jingi na juhudi ambazo aliweka kumwokoa hazikuzaa matunda.
Tangu mauti hayo ya mwanawe, amekuwa akimshutumu na kumlaumu Mungu kwa kuyachukulia maisha kama yasiyokuwa na thamani tena.