Habari

Mwanamke ashtakiwa kupokea Sh30 milioni kilaghai akidai ana laini ya kuuza bidhaa ng’ambo

Na RICHARD MUNGUTI August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MFANYABIASHARA jijini Nairobi ameshtakiwa kwa kumlaghai mwekezaji Dola za Marekani 50,000 (Sh30 milioni) za kumdhamini kuuza bidhaa ughaibuni.

Lilian Wangui Odwoma almaarufu Lilian Weru alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Dolphina Alego.

Wangui alikana kumlaghai Elizabeth Wanjiku Muigai pesa hizo, akijifanya kuwa mwakilishi wa kampuni Pacific Concord International FZC yenye makao yake makuu mjini Dubai.

Wangui anadaiwa alimpa Wanjiku barua ya kumwezesha kutoa bidhaa nchini Kenya na kuiuzia kampuni hiyo ya Pacific Concord International FZC bila bughudha.

Mshtakiwa alikabiliwa na shtaka kwamba kati ya Mei 4 na 20, 2024 katika eneo la Wheatland, Nairobi akishirikiana na watu wengine ambao hawako mahakamani walipokea kwa njia ya ulaghai USD50,000 kutoka kwa Elizabeth Wanjiku Muigai akidai alikuwa na uwezo wa kumdhamini kuuza bidhaa na pia ufadhili kutoka kwa kampuni ya Pacific Concord International FZC iliyoko Dubai kufanya biashara nayo.

Pia Wangui alishtakiwa kwa kupokea pesa zilizopatikana kwa njia isiyo halali.

Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka Hilary Isiakho kwamba Wangui alijifanya kuwa ajenti wa Pacific Concord International FZC nchini Kenya na kwamba alikuwa na uwezo wa kumpa barua ya kupokea ufadhili na wakati huo huo ya kufanya biashara nayo.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh3 milioni pesa tasilimu.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kusikizwa.

Pia hakimu aliamuru mshtakiwa akabidhiwe nakala za ushahidi aandae tetezi zake.